Wajane sasa waomba uwakilishi bungeni - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 24 June 2025

Wajane sasa waomba uwakilishi bungeni


Burhani Yakub, Tanga.


maipacarusha20@gmail.com 


Wajane ni kundi lililosahaulika na kutopewa kipaumbele katika jamii hivyo wameomba ufanyike mchakato wa kupata uwakikishi bungeni ili changamoto wanazokabiliana nazo kila siku ziweze kusikika.


Wametoa ombi hilo katika risala yao iliyosomwa na Katibu wa Chama Cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) Mkoa wa Tanga,Fatuma Madule wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake wajane Duniani iliyofanyika kwa ngazi ya Wilaya ya Tanga katika shule ya Sekondari Usagara jijini hapa.


Amesema wanawake wanapofiwa na wenza wao ndugu wa waume zao wamekuwa wakiwanyang'anya mali zote zikiwamo walizochuma pamoja na kuwaacha na mzigo wa watoto yatima.


"Sisi wanawake wajane tunakabiliwa na madhila makubwa,tunapoondokewa na wenza wetu hujikuta tukifukuzwa kwenye nyumba,tunapokonywa kila kitu,lakini tunaachiwa ulezi wa watoto kuanzia kuwasomesha shule kuwahudumia chakula,mavazi, matibabu na kila kitu ndugu wa waume zetu hawana hata huruma"amesema Madule.


Amesema kutokana na madhila wanayokabiliana nayo wajane wengi hujikuta wakidhoofu kwa kulia peke yao huku wakikosa mahala pa kusemea ndiyo sababu CCWWT inadhamiria kuomba ufanyike mchakato wa kundi lao kupata uwakikishi bungeni.


Mratibu wa maadhimisho hayo Bertha Maqway amesema yameandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo CCWWT lengo likiwa ni kuwapa jukwaa la kukutana na kuzungumzia changamoto wanazokumbana nazo.


"Wanawake wajane ni kundi ambalo kila kukicha linaongezeka lakini pia ni kundi linalokabiliwa na changamoto nyingi na hili tumelishuhudia hapa jinsi walivyotoa ushuhuda wa madhila yanayowakuta baada ya kufiwa na wenza wao"amesema Maqway.


Katika maadhimisho hayo,wajane wa Jiji la Tanga walifanya maandamano yaliyoanzia shule ya Msingi Usagara na kupokewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Dadi Kolimba ambapo pia lilifanyika kongamano.


Akitoa mada katika kongamano la maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa asasi isiyo ya Kiserikali ya Good Samaritan Charitable and Pain Relief (GSCPR)Lulu George amewataka wajane kukubaliana na hali,kumcha Mungu na kuendesha shughuli za ujasiliamali badala ya kunung'unika.


"Nashukuru nyinyi mmejikubali hadi mmefika hapa...hii ni hatua kubwa,kinachotakiwa sasa ni kujikita katika shughuli za ujasiliamali,huku mkifanya ibada kwa sababu nyinyi ni mashujaa mnaohitajika na familia zenu kuziendeleza kiuchumi na kijamii"amesema Lulu.


Akizungumza katika kongamano Hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga amesema Serikali ipo pamoja na wanawake wajane na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto ziliotolewa.


MWISHO





No comments: