Asasi za kiraia zapeleka.mapendekezo CCM - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 22 October 2025

Asasi za kiraia zapeleka.mapendekezo CCM



Na Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com 


Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na mashirika wanachama wake na wadau wengine wa haki na demokrasia wamefanya ziara katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Lumumba, Dar es Salaam, ambapo waliwasilisha mapendekezo muhimu kwa chama tawala kuhusu hali ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. 


Ziara hii ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za AZAKI katika kuhamasisha majadiliano ya kitaifa na maridhiano yenye lengo la kujenga umoja wa kitaifa na kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani, haki na uwazi.


 Wajumbe wa AZAKI walipokelewa na Mheshimiwa Rabia Abdalla Hamid, ambaye ni Katibu wa wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, akiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa John Mongella.


Katika kikao hicho, AZAKI ziliwasilisha hoja nne kuu ambazo ni: 

_(1) Uundwaji wa Tume Huru ya Kiraia kuchunguza matukio ya utekaji na upoteaji wa watu,

 (2) Hali ya demokrasia, uhuru wa AZAKI na vyombo vya habari,

 (3) Uhitaji wa majadiliano na maridhiano ya kitaifa, 

 (4) Uharakishwaji wa mchakato wa Katiba Mpya._


a) *Kuhusu Kukomesha Matukio ya Utekaji nchini*

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na THRDC zikiwemo taarifa za polisi kati ya mwaka 2016 hadi 2025 kumekuwa na matukio takribani 256 ya utekaji na upoteaji wa watu, wakiwemo watoto 96 na watu wazima 160, huku matukio mengi yakihusisha wakosoaji wa serikali, waandishi wa habari, wanaharakati na wanasiasa. 

Kupitia mawasilisho hayo, AZAKI zilisihi kuundwa kwa tume huru ya kiraia itakayochunguza kwa uwazi na haki matukio yote ya utekaji na upoteaji wa watu, pamoja na kuwawajibisha wahusika bila kujali nafasi zao.


Kwa upande wa CCM, Naibu Katibu Mkuu Ndg. John Mongella, alipokea hoja hizo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM na akapongeza AZAKI kwa kuibua mjadala huo muhimu. 

Alieleza kuwa chama kimepokea mapendekezo hayo kwa uzito mkubwa na kitayafikisha ngazi za juu zaidi kwa hatua stahiki.

 Kuhusu hoja ya kuundwa kwa tume huru ya kiraia kwa ajili ya kuchunguza matukio ya utekaji, CCM ilikubaliana na umuhimu wake, wamelipokea na kuahidi kuwa wataangalia namna ya kulifanyia kazi. 

Mongella alisisitiza kuwa chama kinatambua wajibu wake katika kulinda haki za binadamu na kwamba Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari amewahi kutoa tamko kali la kukemea vitendo vya utekaji na upoteaji wa watu, akionesha msimamo wa wazi wa serikali na chama katika kulinda usalama wa raia.

b) *Uhuru wa Azaki , Uhuru wa Kujieleza na Demekrasi* 


Kuhusu hoja ya demokrasia na nafasi ya AZAKI, CCM ilieleza kuwa chama kimekuwa mstari wa mbele kuhimiza mazingira ya kisiasa yenye uhuru na ushiriki mpana wa wadau wote, wakiwemo watetezi wa haki, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla.

 Mongella alibainisha kuwa AZAKI ni wadau muhimu katika kujenga taifa lenye demokrasia imara, na hivyo chama kinatambua mchango mkubwa wa mashirika hayo katika kutoa elimu kwa umma, kufuatilia uwajibikaji wa viongozi na kuchochea mijadala ya kitaifa.

 Alifafanua zaidi kwamba asilimia 80 ya mapendekezo yaliyotolewa na AZAKI tayari yameingizwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025, hatua inayoonesha dhamira ya chama kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wa kiraia.

c) *Maridhiano ya Kitaifa na Katiba Mpya*

Hoja ya tatu iliyowasilishwa na AZAKI ilihusu umuhimu wa majadiliano na maridhiano ya kitaifa kabla na baada ya uchaguzi mkuu, ili kuhakikisha umoja wa Watanzania unalindwa na misingi ya amani inadumu.

 CCM kupitia Naibu Katibu Mkuu ilikubaliana na hoja hiyo na kueleza kuwa majadiliano ya kitaifa ni nyenzo muhimu katika kujenga umoja, maridhiano na kuimarisha utawala wa sheria.

 Mongella alisema kuwa chama kinaunga mkono mazungumzo ya aina hiyo, hususan katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, na kwamba CCM iko tayari kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mfano wa amani na umoja barani Afrika.


Kwa hoja ya Katiba Mpya, CCM ilisisitiza kuwa chama kimeendelea kubeba ajenda hiyo kwa dhati, jambo linalodhihirishwa na kujumuishwa kwake katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025. 

Mongella alieleza kwamba endapo CCM itashinda uchaguzi ujao, kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kutakuwa miongoni mwa vipaumbele vya kwanza vya serikali itakayoundwa. Aliongeza kuwa chama kinaona umuhimu wa kupata Katiba Mpya inayojengwa juu ya misingi ya ushirikishwaji wa wananchi na inayojibu mahitaji ya sasa ya taifa, bila kuvunja misingi ya amani na umoja uliopo.


CCM imesisitiza kuwa itapendelea kuwa karibu na AZAKI kwa kuwa maoni ambayo wamekuwa wakiyaleta mengi pia ndio malengo ya CCM kwa Watanzania. Kwa ujumla, kikao hiki kimedhihirisha dhamira ya wazi kati ya AZAKI ya kujenga taifa lenye amani, haki, umoja na maridhiano. 

THRDC na wadau wake wamesisitiza kuwa wataendelea na ziara zao kwa vyama na taasisi nyingine ili kuhimiza umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa, kulinda democrasia, hali za watu huku CCM ikiahidi kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo, demokrasia na haki kwa Watanzania wote.


Imetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania 

22 Oktoba 2025

No comments: