Viongozi wa dini kanda ya Kaskazini waibua hoja saba kuelekea uchaguzi mkuu, wataka amani , haki na busara kwa vyombo vya dola - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 22 October 2025

Viongozi wa dini kanda ya Kaskazini waibua hoja saba kuelekea uchaguzi mkuu, wataka amani , haki na busara kwa vyombo vya dola




 






Mwandishi wetu, Moshi


maipacarusha@gmail.com 


Kongamano la amani la viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali kanda ya kaskazini, limeibua hoja saba kuelekea uchagaguzi mkuu wa Octoba 29 mwaka huu, huku likitaka vyombo vya dola kujitahidi kutumia busara na hekima kuelekea uchaguzi mkuu .

Wakizungumza katika kongamano hilo, lililofanyika katika ukumbi wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzaniania(KKKT) wa Uhuru hosteli, mjini Moshi Masheikh, Maaskofu, Mapadri na wachungaji wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, kwa Pamoja walisisitiza watanzania kulinda amani, katika uchaguzi mkuu na kutaka kupuuzwa wale wote wanaohubiri ama kuhamasisha vurugu.

Akisoma maazimio ya kongamano hilo, baada ya viongozi wa dini kutoa maelekezo yao kuelekea uchaguzi mkuu,, Katibu wa Baraza kuu la Waislam, (BAKWATA) mkoa wa Kilimanjaro, Alhaji Awadhi Lema wamekubaliana viongozi na wananchi wote kuwahamasisha watu wote waliojiandikisha kupiga kura kuhakiki majina yao na kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Alhaji Lema alisema pia wameazimia kuendelea kufanya Makongamano ya amani ili kuendelea kuwakumbusha watanzania mara kwa mara umuhimu wa kulinda amani.

“katika kongamano hili pia tumekubaliana kuwa ni vizuri vyombo vya dola kuendelea kutumia hekima na busara katika kulinda amani hasa siku ya uchaguzi”alisema


Viongozi wa dini

Alisema pia wameazimia Viongozi wa dini wawaelimishe waumini kuhusu haki na wajibu wao katika kulinda amani na Kuwahimiza watanzania wote kuepuka uchochezi katika mitandao ya kijamii ama vyombo vingine vya habari.

“Pia tumependekeza kupanuliwe wigo wa ushiriki wa viongozi wa kidini katika vyombo vya utungaji wa sheria ama kufanya uamuzi na tumekubaliana kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kulinda amani wakati wa kudai haki”alisema

Wakizungumza katika kongamano hilo, Sheikh wa mkoa wa Kilimanjaro sheikh Shaban Mlewa na Sheikh wa mkoa Arusha, Sheikh Shaban Juma, kwa Pamoja walitaka watanzania kujitahidi kwa kila hali kulinda amani na utulivu uliopo nchini.

Sheikh Mlewa alisema kuna mengi ya kujifunza katika nchi mbali mbali ambazo zilikuwa na amani lakini sasa zimeingia katika machafuko makubwa na Imani imekuwa ngumu kurejea.

“Ni muhimu sana Watanzania kuwa wazalendo kwa kupenda nchi yao, kupendana, kusameheana na kuwa waadilifu ili kuendelea kuenzi amani na utulivu uliopo sasa”alisema

Sheikh wa mkoa Arusha, Sheikh Shaban Juma amesema hakuna haki kama hakuna amani, kwa sababu sehemu ambayo haina amani ni vigumu haki kupatikana.

“Amani inajengwa kwa misingi mikuu mitatu, ambayo ni kumtambua Mwenyezimungu, kutambua nafsi yako na kulinda haki na uhai wa watu wengine”alisema

Alisema uchaguzi mkuu usiwafanye watanzania kukimbia nchi yao, kwa kukosa amani hivyo ni muhimu sana watanzania kutumia haki yao kujitokeza katika uchaguzi kuchagua viongozi ambao wanawataka bila hofu wala vurugu.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Askofu Mkuu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini, Wakili Mchungaji Daniel Swai alisema, ni muhimu sana kila mtanzania kutambua na kuilinda haki yake ikiwepo haki ya kupiga kura.

Alisema ni makosa makubwa mtu yoyote kujitokeza na kuhamasisha watu wengine kutotimiza wajibu wao wa kupiga kura.


Hata hivyo, alihimiza haki na amani na kueleza haki ni utoaji wa kitu kwa usawa, kitu kilichostahiki na cha kweli kwa kila mtu nakueleza amani na Haki ni vitu ambavyo vinakwenda Pamoja.

Msaidizi wa Askofu Mkuu jimbo la Katoliki la Moshi, Padri Deogratias Matiika amesema  ni muhimu sana kulinda amani iliyopo lakini pia kuzingatia utoaji wa haki sawa kwa wote.

“Lazima tulinde haki za watu, viongozi wetu waheshimu wananchi lakini pia na wananchi waheshimu viongozi, kwani katika siku za karibuni kumeibuka mambo ambayo si sawa kwa wananchi kutukana matusi viongozi katika mitandao ya kijamii”alisema

Padri Matiika alisema viongozi wanapaswa kulinda haki na kama haki isipokuwepo katika jamii taifa litakwenda pabaya na hivyo ni muhimu pia kusali kila mara kuombea haki katika taifa.

Kwa upande wake, Padri Francis Mahimbo wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga, alitaka haki za watu kuendelea kulindwa katika taifa na kujenga tabia ya kuvumiliana.

Alisema msingi wa amani ni haki na hivyo ni muhimu sana katika taifa haki za watu kulindwa ili Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu”alisema

Katika kongamano hilo, lilihudhuria pia na viongozi wa kamati za dini za vijana na wanawake, ambazo kwa Pamoja zilitaka watanzania kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu na kutengwa viongozi ama watu wanaochezea vurugu na uvunjwaji wa sheria.

MWISHO
 


 

No comments: