MIRERANI IPO SALAMA KWA DIWANI SALOME MNYAWI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 28 October 2025

MIRERANI IPO SALAMA KWA DIWANI SALOME MNYAWI




Na Mwandishi wetu, Mirerani 


maipacarusha@gmail.com 


MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Salome Nelson Mnyawi, amewaomba wakazi wa eneo hilo kumpa kura nyingi za ndiyo kwani amefanikisha maendeleo mengi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.


Salome akizungumza kwenye eneo la Maduka Matatu, Mtaa wa Twiga, Kata ya Mirerani, amesema alichaguliwa kwa mara ya kwanza kipindi kilichopita hivyo anaomba kipindi kingine cha miaka mitano ili aweze kushirikiana nao kufanikisha maendeleo ya eneo hilo.


Ameeleza baadhi ya mafanikio yaliyofanyika kwenye kipindi chake ni ujenzi wa kituo cha afya Tanzanite ambapo kimekamilika na sasa kinasubiria kufunguliwa na kutoa huduma kwa jamii.


"Pia miundombinu ya barabara za lami kutoka soko la getini hadi lango la kuingia na kutoka ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite pamoja na taa na barabara kutoka transifoma hadi kituo cha mafuta cha Kibobo," amesema Salome.


Amesema sekta ya elimu wameongeza madarasa katika shule za msingi Songambele na Tanzanite na wanafunzi wenye mahitaji maalumu wamejengewa madarasa na mabweni ya kulala.


Amesema anaomba kipindi kingine cha miaka mitano ili aendeleze mambo mengine mazuri zaidi katika sekta mbalimbali..


"Naombeni kura zote za ndiyo, namuombea mgombea ubunge wa CCM James Ole Millya na mgombea urais Mama yetu kipenzi Dkt Samia Suluhu Hassan tumpe kura zote za ndiyo Oktoba 29 mwaka huu wa 2025," amesema Salome.


Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni akimnadi mgombea udiwani huyo Salome amesema ni mwana mama mahiri mwenye uwezo wa kuwaongoza wana Mirerani kwa miaka mingine mitano.


"Siku ya jumatano Oktoba 29 mwaka huu wa 2025 tunatiki kwa Diwani Salome, tunatiki kwa Mbunge Millya na tunatiki kwa Rais Dkt Samia, mapema sana," amesema Makeseni.


Baadhi ya waliokuwa watia nia wa kata hiyo ambao kura zao hazikutosha wameeleza kwamba Salome ni chagua sahihi kwa wana Mirerani hivyo apewe kura zote za ndiyo.


Mmoja kati ya waliokuwa watia nia Juma Selemani amesema Salome ameacha alama kubwa ya uongozi kwa hiyo anastahili kupata kipindi kingine.


Aliyekuwa mtia nia mwingine wa kata hiyo ackson Ochieng' amesema Mungu ndiye anampa uongozi mtu anayemtaka hivyo Salome apewe kura zote za ndiyo.


MWISHO

No comments: