Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WANANCHI Mil 2.1 waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Morogoro wamehimizwa kujitokeza kupiga kura Octoba 29,2025(kesho) katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na alieleza taarifa ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais ,wabunge na madiwani yamekamilika.
"Maandalizi yote yamekamilika pamoja na vitendea kazi kufika katika maeneo yote yaliyopangwa kwaajili ya zoezi hilo,"alisema.
Alisema ana imani kuwa wananchi zaidi ya milioni 2,100,000 wote watapiga kura, hakuna sababu awe umejiandisha alafu usiende kupiga kura.
Malima alisema kwa mkoa wa Morogoro kuna vituo 5860 vya kupigia kura na kuwataka waajiri kuwaruhusu watumishi wao kwenda kupiga kura katika maeneo waliojiandikisha ili kutumia haki yao ya msingi.
Malima alisema wamezingatia kuweka mazingira mazuri kwa makundi maalumu kama watu wenye ulemavu, wajawazito na wazee huku akisisitiza wananchi kuwahi kupiga kura mapema ambapo alisema vituo vitafunguliwa saa 1 asubuhi na kuhitimisha saa kumi jioni.
Alisisitiza kuwa usalama na amani vimezingatiwa na kuwataka wananchi kufika katika maeneo ya kupigia kura na kuondoka badala ya kuzagaa zagaa katika maeneo hayo.
Hata hivyo alisema kwa mkoa wa Morogoro hakuna tukio lolote la kuashiria uvunjifu wa amani na kuwasisitiza wananchi wa mkoa huo kuwa zoezi la kupiga kura ni furaha na sio karaha.
Katibu tawala Mkoa wa Morogoro Dk Mussa Ali Mussa aliwaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu pindi watakapo kuwa wakisubiri matokeo na hiyo ni kutokana na Mazingira na jiografia ya mkoa ambao una milima mingi.
"Kutokana na maeneo ya milimani ya mkoa wetu wa Morogoro, matokeo yanaweza kuchelewa lakini tuwe wavumilivu,"alisema Dk Ali Mussa.
Baadhi ya vijana katika manispaa ya Morogoro walisema kuwa kwa mazingira wanayoishi wamezoea kujitafutia riziki kwa amani na utulivu na kwamba hawahitaji vurugu zozote.
"Sisi tunajitafutia riziki za kila siku bila shida yoyote, tunataka amani iendelee ili tuweze kuendesha maisha yetu na familia zetu"alisema Issa Juma.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment