Na Mwandishi Wetu
maipacarusha20@gmail.com
Mabalozi wanaowakilisha mataifa na taasisi za kimataifa nchini, wamethibitisha kwa kauli moja dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi.
Hayo yamejiri leo, Ijumaa Novemba 28, 2025 katika Mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Jumuiya ya Wanadiplomasia wanaowakilisha mataifa na taasisi mbalimbali nchini.
Wanadiplomasia hao, wamesema wanaiona Tanzania kama mshirika muhimu, imara na wa kuaminika katika diplomasia ya kikanda na kimataifa.
Pia, wamesema wametambua juhudi zinazofanywa na Serikali kurejesha umoja wa Taifa baada ya matukio ya Oktoba 29, na wametoa pongezi kwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuimarisha amani, utawala bora na ustahimilivu wa kitaifa.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi Kombo amewahakikishia mabalozi hao kuwa, Tanzania itaendeleza ushirikiano wa manufaa kwa pande zote.
Ametumia fursa hiyo kuwapa taarifa kuhusu mwenendo wa uchaguzi mkuu, matukio yaliyojitokeza baadaye na hatua ambazo Serikali imechukua ikiwemo kulinda maisha na mali za wananchi, kurejesha utulivu na kuendeleza huduma za kijamii na uchumi bila kusuasua.

No comments:
Post a Comment