Wahitimu 150 Tanga na Kilimanjaro kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 14 November 2025

Wahitimu 150 Tanga na Kilimanjaro kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi

Mkurugenzi wa City Institute Dar es salaam Shabani Mwanga alitoa vyeti vya kuhitimu masomo ya miaka miwili ya ufundi stadi Veta Tanga


 Mkurugenzi wa City Institute Dar es salaam Shabani Mwanga akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Chuo cha ufundi stadi Veta Tanga na viongozi wa Chuo hicho.

Mkurugenzi wa City Institute Dar es salaam Shabani Mwanga akizungumza wakati wa mahafali ya 49 ya wahitimu wa Chuo cha ufundi stadi Veta Tanga



Burhani Yakub,Tanga.


maipacarusha@gmail.com 


Vijana 150 waliohitimu darasa la saba pamoja na Sekondari wa mikoa ya Tanga na Kilimanjaro wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi baada ya kujitokeza kwa mfadhili aliyeamua kugharamia masomo yao katika chuo cha ufundi stadi Veta kilichopo Jijini Tanga.


Mkurugenzi wa City Institute Dar es salaam,Shabani Mwanga ametoa ahadi hiyo wakati wa mahafali ya 49 ya wahitimu wa chuo cha ufundi stadi Veta Tanga kilichopo Jijini hapa.


Mwanga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesema vijana 100 wa kutoka vijiji na Wilaya zilizopo Mkoa wa Tanga watakaowahi kujiandikisha kuomba kusoma katika chuo cha Veta Tanga msimu utakaoanza Januari mwakani atawalipia ada na gharama nyingine.


"Lengo ni kuwahamasisha vijana wazawa wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kusoma Veta Ili wapatikane mafundi wa fani mbalimbali watakaoahiriwa na kujiajiri hatimaye kupunguza ombwe la vijana wasiokuwa na ajira.


Sababu nyingine iliyomsukuma kutoa ufadhili huo kwa vijana wa Tanga amesema ni kitendo cha kutoafanya maandamano na vurugu wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika kama ilivyofanyika katika majiji na miji mingine nchini Tanzania.


"Mkoa wa Tanga ulikuwa na utulivu kipindi ambacho vijana wa miji na majiji mengine waliendesha maandamano na vurugu zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu...hii imenivutia sana na nimemua kutoa ufadhili Ili wapate ujuzi endelevu"amesema Mwanga.


Mkurugenzi huyo amesema ameamua kugharamia ada na gharama za bweni za vijana 50 kutoka Kilimanjaro watakaojiandikisha katika chuo cha Veta Tanga ikiwa ni njia ya kuenzi Mkoa aliozaliwa.


"Ili na vijana wa nyumbani kwetu Kilimanjaro wasijisikie vibaya nitachukua 50 watakaojiandikisha katika chuo cha ufundi stadi Veta Tanga nitagharamia ada za masomo na bweni lakini kipaumbele kwa wote wa Tanga na Kilimanjaro kiwe kwa wasichana na wenye ulemavu"amesema Mwanga.


Mwanga pia ameahidi kuwalipia ada za mitihani wanafunzi 16 ambao ilikuwa washindwe kufanya mitihani kitaifa ya kuhitimu masomo ya miaka miwili inayotarajiwa kuanza Disemba mosi 2025.




Katika kuenzi uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi huyo ameahidi kufadhili jumla ya kompyuta 20 kwa ajili ya masomo kwa vitendo ya wanafunzi wa chuo hicho.


"Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyemudu kuliongoza Taifa katika kipindi kigumu bila kutetereka na kwa sababu hiyo kama mdau wa elimu ni jukumu langu kumuunga mkono kwa kusaidia kidogo nilichonancho"amesema Mwanga.


Mkuu wa Chuo cha ufundi stadi Veta Tanga, Gideon Olelairumbe amesema itakuwa ni mara ya pili kwa Mwanga kufadhili kompyuta ambapo mwaka jana alitoa pia kompyuta 20 ambazo zinatumika kuwafundishia wanafunzi chuoni hapo.


Chuo cha ufundi stadi Veta ambacho kilianzishwa mwaka 1975 kimekuwa kikitoa kozi ndefu na fupi za fani mbalimbali za ufundi ambapo wahitimu wameweza kujiajiri na kuajiriwa katika maeneo tofauti ndani na na nje ya Tanzania.


"Wahitimu hawa walianza masomo Januari mwaka 2024 wakiwa 361 wavulana wakiwa 216 na wasichana 145 hapa walipo ni mafundi wa fani mbalimbali ambao wamepikwa kikamilifu"amesema Olelairumbe


MWISHO

 

No comments: