Na Mwandushi wetu
maipacarusha@gmail.com
Muda mfupi baada ya Uzinduzi wa kampeni ya Shangwe la Sikukuu na TANAPA - Msimu wa pili ndani ya Hifadhi ya Taifa Katavi idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje wameonyesha kuvutiwa na kuamua kufanya utalii wa ndani leo Desemba 20, 2025 huku wakieleza kuridhishwa na kufurahishwa na vivutio, mandhari na maajabu ya uumbaji yaliyomo ndani ya eneo hilo.
Miongoni mwa maeneo maarufu waliyoonyesha kuvutiwa nayo ni pamoja na “Paradise” eneo linalofananishwa na bustani ya paradiso inayoelezwa katika maandiko matakatifu ya biblia. Eneo hilo lina hali ya utulivu huku likisheheni wanyamapori wengi kama vile makundi makubwa ya nyati, twiga, tembo, simba, pundamilia, swala bila kusahau aina mbalimbali za nyoka, mnyama ambaye anasifika sana kwa udanganyifu.
Maeneo mengine ni pamoja na uwanda wa Katsunga unaotumika kama ghala la chakula kwa wanyamapori hao kipindi cha kiangazi, bwawa la viboko almaarufu “Ikuu” pamoja na mti wa mzimu wa Katabi ambao hutumika na watu wa kabila la wagongwe, wapimbwe na wabende kufanya matambiko ya asili kuomba mahitaji mbalimbali.
Akizindua Kampeni hiyo, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini Steria Ndaga kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA alisema, “Kampeni ya *“Shangwe la Sikukuu na TANAPA”* ni jitihada za kujitangaza ndani ili kukuza utalii na kuongeza idadi ya watalii watakaoliongezea Taifa mapato.”
![]() |
Aidha, Kamishna Ndaga aliongeza kuwa TANAPA imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, malazi pamoja na maeneo ya kutolea taarifa mbalimbali (VIC) kwa wageni ili kuvutia watalii pamoja na wawekezaji, kwani msingi mkubwa wa uwekezaji ni miundombinu imara, sera bora na maeneo sahihi ya uwekezaji ambayo TANAPA ina sifa hizo.
Mbunge wa Mpanda Mhe. Haidary Sumry aliwahimiza wananchi wa mkoa wa Katavi na mikoa ya jirani kutembelea Hifadhi ya Taifa Katavi hususani kipindi hiki cha mapumziko ambacho familia nyingi huwa pamoja ili kujionea vivutio mbalimbali kama alivyofanya yeye na familia yake.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Katavi, Dr. Emilian Kihwele akiwakaribisha wageni hao alisema kuwa kampeni hii imeonyesha mwelekeo chanya kwani hifadhi leo imepokea zaidi ya watalii 130 waliotembelea Hifadhi hii na kujionea mandhari tofauti na zinazovutia, wanyamapori mbalimbali na maeneo ya uwekezaji.
![]() |
Uzinduzi wa Kampeni hiyo pia umehudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Halimashauri ya Mpimbwe Bi. Shamimu Mwariko, Makamishna wa Uhifadhi TANAPA, viongozi waandamizi wa chama na serikali, wadau wa utalii na wanufaika mbalimbali wa uhifadhi na utalii katika Hifadhi ya Taifa Katavi.




No comments:
Post a Comment