![]() |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MCHUMI Mwandamizi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) Emanuel Lazaro amesema katika kuimarisha uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma,kupitia mpango mkakati wake itaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali ili waweze kuelewa kwa kina ripoti zake za ukaguzi
Emanuel alieleza hayo alipowasilisha mada kuhusu njia na aina za ukaguzi wakati wa mafunzo ya ukaguzi kwa waandishi wa habari mkoani Morogoro,yaliyoandaliwa na ofisi hiyo ya NAOT.
Alisema Miongoni mwa mpango mkakati unaokuja wa Ofisi hiyo ni kujielekeza kuhakikisha inaandaa taarifa ambayo ni rafiki kwa kila mmoja na inawafikia wadau wote wakiwemo watu wenye ulemavu wa uoni hafifu.
Mchumi huyo mwandamuzi alisema kuwa watu wenye ulemavu wa uoni hafifu wanahitaji kupata ripoti zilizopo kwenye karatasi za nukta nundu.
"Kwa Sasa Ofisi ya NAOT imejielekeza kuandaa ripoti ambazo ni za nukta nundu ili wenzetu nao waweze kufikiwa kwa urahisi,"alisema.
“ Lengo la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuandaa ripoti kama hiyo ni kwa ajili ya wale watu wenye ulemavu wa uoni hafifu nao wanaweza kusoma na kujua ,pia nini kwenye ukaguzi wake CAG aliona na ameishauri nini Serikali,”alisema Emanuel.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, Mkaguzi Mkuu wa Nje (CEA),mkoa wa Morogoro, Baraka Mfugale alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Mfugale alisema mpango huo mkakati unalenga kuimarisha ushirikishaji wadau , hususan Vyombo vya Habari ,katika mchakato wa uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma.
Alisema Mpango mkakati huo unatambua kuwa Vyombo vya habari ni kiungo muhimu kati ya taarifa za ukaguzi na wananchi kwa kuwa ndivyo vinavyobeba jukumu la kuifafanua , kuichambua na kuifikisha taarifa hiyo kwa umma kwa lugha rahisi na inayoeleweka.
Mfugale alisema Ofisi hiyo imejipanga kuendelea kuboresha uwazi katika utoaji wa taarifa za ukaguzi ,kuimarisha mawasiliano na wadau, na kujenga uelewa mpana kuhusu kazi , majukumu na mipaka ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
“Mafunzo haya ni ushahidi wa vitendo wa dhamira hii , yakilenga kuongeza uwezo wa Waandishi wa Habari katika kusoma, kuchambua na kuripoti kwa usahihi ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali “ alisema Mfugale.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi hiyo , Focus Mauki alisema, Ofisi inaamini mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi wa kuuliza maswali ya kitaalamu , kufanya uchambuzi wa kina na kuibua mijadala chanya inayosaidia Serikali , Bunge na taasisi nyingine kuchukua hatua staahiki kulingana na mapendekezo ya ukaguzi.
Mauki alisema mafunzo yametolewa kwa waandishi wa habari, Asasi za Kiraia na makundi na kwa waandishi wa habari ni mikoa ya Dar es Salaam, Arusha , Shinyanga, Mtwara, Tanga , Kilimanjaro , Manyara, Tabora, Iringa, Ruvuma , Lindi , Rukwa, Njombe , Mbeya , Mwanza , Mara , Dodoma , Pwani na Morogoro.
“ Kwa Morogoro ni mwendelezo wa juhudi hizo yakilenga kuhakikisha waandishi wa habari wa mikoa yote wanapata uelewa sawa kuhusu kazi za ukaguzi na matumizi ya ripoti ya CAG katika kuimarisha uwajibikaji wa umma” alisema Mauki.
Mwisho.




No comments:
Post a Comment