Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
TUKIO la kuchomwa moto kwa magari mawili katika kijiji cha Lusanga, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro linafanyiwa uchunguzi na jeshi la polisi, baada ya ndugu wa marehemu Mwanahasan Juma Hamis(18) kutoridhishwa na kifo Cha ndugu yao.
Taarifa ya iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, ilisema tukio hilo limetokea Desemba 17, 2025 baada ya mwili wa marehemu uliposafirishwa kwenda kijijini kwao kwa ajili ya mazishi na mwajiri wake ukitokea jijini Dar es Salaam alipokuwa akifanya kazi.
Kamanda Mkama alisema magari hayo yalitumika kusafirisha mwili wa marehemu aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa Miraji Chomoka ambapo alifariki kwa maradhi jijini Dar es salaam.
Hata hivyo, wakati taratibu za mazishi zikiandaliwa ilitokea taharuki iliyohusishwa na kutiliwa mashaka ya Mazingira ya kifo cha marehemu, hali iliyopelekea kuwafungia ndani wasindikizaji wa msiba na kuchoma moto magari waliyosafiri nayo wakiwataka watoe maelezo zaidi.
"Mvutano uliibuka baada ya ndugu wa marehemu kudai kuwepo kwa sintofahamu juu ya hali ya mwili wa marehemu, madai yaliyosababisha hasira kwa baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Kilingeni Kijiji cha Lusanga Kata ya Diongoya waliofika msibani,"alisema.
Alisema Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya mtaa walifanikiwa kuwaokoa wasindikizaji wa msiba huo.
Aidha upande mwingine wa taarifa hiyo ya polisi unadai kuwa mwili huo ulikuwa umefanyiwa taratibu za kitabibu ikiwemo uchunguzi, jambo ambalo linaendelea kufanyiwa kazi ili kubaini ukweli wake.
Kamanda huyo wa polisi aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuacha kuchukua sheria mkononi huku wakiahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi kukamilika.
Jeshi la polisi linaendelea kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Katibu wa hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro Scholastica Ndunga alithibitisha hospitali hiyo kupokea mwili wa marehemu.
Alisema uchunguzi tayari umefanyika na kwamba matokeo ya uchunguzi huo utatolewa na jeshi la polisi kwani wao ndo wenye mamlaka.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment