MBUNGE WA BUTIAMA DKT. WILLSON MAHERA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA KATA YA BURUMA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 11 December 2025

MBUNGE WA BUTIAMA DKT. WILLSON MAHERA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA KATA YA BURUMA

 




Na Onesmo Mbise, Butiama.


Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Willson Charles Mahera, ameendelea na ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Buruma kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa miradi unakwenda kwa kasi, ubora na viwango vinavyotakiwa.


Katika ziara hiyo, Dkt. Mahera ameanza kwa   kukagua daraja la Rwako lenye thamani ya shilingi milioni 22, ambapo ujenzi unaendelea vizuri, ambapo akiwa hapo  alijadiliana na watendaji pamoja na wakandarasi kuhusu maboresho yanayohitajika ili kuongeza ufanisi na kuharakisha kukamilika kwa daraja hilo muhimu kwa wananchi.


Akiendelea na ziara  Shule ya Msingi Kurugese, ambako ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo unaendelea kwa gharama ya shilingi milioni 70.1,  Mbunge amesisitiza umuhimu wa kazi kufanyika kwa kuzingatia viwango ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.


Katika Shule ya Msingi Ibiso, Dkt. Mahera amekagua ujenzi wa madarasa manne pamoja na matundu sita ya vyoo yanayogharimu shilingi milioni 157.3, ambapo ametoa  ushauri wa kuboresha ubora wa kazi na kuimarisha usimamizi, huku akiahidi kurejea katika kata ya  Buruma tarehe 15 Januari 2026 kufuatilia hatua za utekelezaji wa ushauri alioutoa. 


Mhe. Mbunge amehitimisha ziara yake katika Shule ya Msingi Ryamgabo, ambako alikagua ujenzi wa madarasa manne yenye thamani ya shilingi milioni 87, na  kuzungumza na Mwalimu Mkuu na kamati za ujenzi kuhusu mbinu za kuharakisha kazi na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.


Mbunge huyo amewapongeza Viongozi wa shule, kamati za ujenzi na viongozi wa eneo hilo kwa ushirikiano na uwajibikaji wao katika kuhakikisha miradi ya elimu inatekelezwa ipasavyo. 


Dkt. Mahera amesisitiza kuwa Serikali na Ofisi yake wataendelea kufuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha inaleta manufaa kwa wanafunzi na jamii nzima ya Butiama.


Dkt. Mahera anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo katika Jimbo la Butiama ambapo leo anatarajia kufanya ziara yake katika kata ya Mirwa na kuzindua mashindano ya mpira wa miguu pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.

No comments: