Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
MAMLAKA ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imewapatia zawadi ya vyakula, mbuzi na fedha taslimu, watoto yatima na waliokuwa wanaishi katika mazingira hatarishi wa kituo cha Light In Africa kwenye kusherehekea sikukuu ya Christmas na mwaka mpya wa 2026 kwa tabasamu.
Afisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, (TEO) Isack Mgaya akizungumza wakati akikabidhi vyakula hivyo ameeleza kwamba gharama walizotumia kuwapatia tabasamu watoto hao ni shilingi 1,847,000.
Mgaya amesema lengo lao ni kuwapa tabasamu kwenye sikukuu ya Christmas na mwaka mpya wa 2026 watoto hao wa kituo cha Light In Africa ambao ni yatima na waliokuwa wanaoishi katika mazingira hatarishi washerehekee kwa furaha.
Amesema pamoja na kuwapa fedha taslimu shilingi 220,000 wametumia shilingi 1,627,000 katika kununua mahitaji mbalimbali ikiwemo mbuzi mmoja, nyama kilo 10 na vyakula kwa ajili ya kusherehekea sikukuu hizo za mwisho wa mwaka.
Ameeleza kwamba wamewapatia mchele kilo 50, sukari kilo 50, kuku 20, mafuta lita 20, ndizi mkungu mmoja, viazi debe mbili, sharubati katoni saba na maji katoni 10.
"Pia tumekabidhi matunda, machungwa 180, mananasi 12, matikiti nane, maziwa ya watoto, ndizi mbivu vichane tisa na lawalawa pakiti mbili," amesema Mgaya.
Mwakilishi wa benki ya CRDB Tawi la Mirerani, Maria Rwezaura amesema wamechangia kiasi cha fedha katika msaada huo ili kurejesha tabasamu kwa watoto hao yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Rwezaura ameeleza kwamba kupitia CRDB wameweza kuchangia kiasi cha fedha baada ya viongozi wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani kuwasilisha ombi la kusaidia watoto hao yatima na waliokuwa wanaishi katika mazingira hatarishi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Oloshonyokie, Lazaro Sanagi amesema wamesaidia watoto hao yatima ili nao washerehekee sikukuu za mwisho wa mwaka wakiwa na furaha.
"Kupitia msaada huu watoto hawa yatima na waliokuwa wakiishi katika mazingira hatarishi watafurahia sikukuu za mwisho wa mwaka," amesema Sanagi.
Mmoja kati ya watumishi wa kituo cha Light In Africa, Jasmine Kimaro amewashukuru viongozi hao wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani kwa kutoa msaada huo kwa watoto hao.
"Tunawashukuru viongozi viongozi hawa kwa kuwajali watoto hawa ambao watasherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa furaha," amesema Kimaro.
MWISHO

No comments:
Post a Comment