Watoto 800 wafanyiwa upasuaji wa viungo Kafika House ,Arusha .Taasisi ya Friedkin yapongezwa kwa ufadhili wa matibabu. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 25 December 2025

Watoto 800 wafanyiwa upasuaji wa viungo Kafika House ,Arusha .Taasisi ya Friedkin yapongezwa kwa ufadhili wa matibabu.




Mwalimu mlezi akiwaelekeza watoto hao taratibu za mchezo 



Mussa Juma,Arusha

maipacarusha@gmail.com.


Watoto 800 waliokuwa na ulemavu wa viungo, wamefanyiwa upasuaji na kupona katika Kituo cha Kafika house kilichopo Arusha, wakiwepo watoto zaidi ya 100 kutoka wilaya ya Meatu,mkoa wa Simiyu.


Watoto kutoka wilaya ya Meatu, wamefanyiwa upasuaji huo wa ulemavu wa viungo, kutokana na ufadhili wa Taasisi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) ambayo kampuni zake kadhaa ikiwepo Mwiba Holding Ltd zimewekeza katika wilaya hiyo, katika shughuli za Utalii wa picha na hoteli, katika eneo la kijiji cha Makao na eneo la pori la akiba la Maswa.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho ambaye pia ndiye  mwanzilishi wa Kituo hicho, Sarah Rejman  alisema tangu kituo hicho, kuanzishwa mwaka 2008 kimewafanyia upasuaji watoto 12,000.


Rejman alisema, Kituo hicho kinatoa  matibabu ya watoto, kufanyiwa upasuaji na kilianzishwa baada ya kuona kuna mahitaji ya watoto kupata sehemu za kukaa kupata matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji kwa kushirikiana na hospitali kadhaa mkoani Arusha.


" Kwa sasa Kituo kina jumla ya watoto 155, wapo waliofanyiwa upasuaji, wengine wanasubiri upasuaji, wapo wanaofanya mazoezi baada ya upasuaji na  kuna watoto wawili wanatarajiwa kurejea nyumbani hivi karibuni baada ya kupona"alisema


Rejman alishukuru sana Taasisi ya Friedkin Conservation Fund, kwa kuendelea kufadhili matibabu ya watoto kutoka wilaya ya Meatu  ambao baadhi wamerejea majumbani na wengine wanaendelea na matibabu.


Watoto wakicheza kama sehwmu ya mazoezi

Baadhi ya watoto kutoka wilaya ya Meatu, ambao bado wapo katika kituo hicho,  baada ya kufanyiwa upasuaji, waliishukuru sana taasisi ya FCF kupitia kampuni yake ya Mwiba Holding Ltd kwa kugharamia matibabu yao, ikiwepo kuwasafirisha kutoka Meatu hadi Arusha.


Madeleke Duda mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya Msingi Makao, Emmanuel Sita ambaye anasoma darasa la Sita shule ya msingi Sakasaka ,Meatu na Noni Zengo ambaye anasoma shule ya msingi Mwangudo darasa la sita, walisema wanashukuru ufadhjli wa matibabu na sasa wameanza mazoezi ya kutembelea baada ya kufanyiwa upasuaji.


Wanafunzi hao, ambao mwezi septemba waliagwa na Mkuu wa wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura kutoka Meatu kwenda Arusha, kwa ajili ya Matibabu hayo, walisema bila msaada wa kampuni ya Mwiba na FCF wasingekuwa na uwezo wa kupatiwa matibabu hayo.


Noni Kulwa alisema sasa wameondokana na ulemavu na watarejea katika masomo, wakiwa wanajiamini na wanauhakika wa kufanya vizuri katika mitihani yao.


Watoto mapacha Kulwa Musa na Doro Musa(12) kutoka  kijiji cha Mbaragane wilaya ya Meatu, ambao tayari wamefanyiwa upasuaji wa miguu,pia walishukuru Mwiba Holding Ltd na FCF kwa kuwasaidia kupata matibabu hayo.


Jackline Lekule ambaye ni mtaalam wa tiba kwa vitendo katika kituo hicho, (occupation therapist) alisema kituo hicho, kinatoa matibabu ya upasuaji wa mguu vifundo, Matege, mdomo Sungura na majeraha ya moto.


Lekule alisema ulemavu huo unasababishwa na changamoto mbali mbali, ikiwepo unywaji wa maji yenye madini mengi ya Floride, upungufu wa vitamin kwa akina mama wajawazito, ugonjwa wa kurithi na watoto kupata majeraha ya moto.


Mmoja wa wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji katika kituo hicho, Rehema Daudi alipongeza kituo cha Kafika kwa huduma bora ambayo wanatoa.


"Mimi mtoto wangu Dorcas Mathias  alikuwa na changamoto ya Nyonga kushuka chini hadi kwenye magoti na hivyo kushindwa kutembea lakini tayari amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri"alisema.


Mkurugenzi wa miradi wa taasisi ya Friedkin, Aurelia Mtui alisema, wataendelea kugharamia matibabu kwa watoto wenye ulemavu chini ya miaka 17 kutoka katika wilaya hiyo ya Meatu.


Mtui alisema licha ya kugharamia matibabu kwa watoto hao, taasisi hiyo pia inagharamia usafiri wa wanafunzi kwenda shule, inatoa chakula cha bure shuleni, imejenga madarasa, nyumba za walimu, vituo vya afya, vituo vya kuzuia wanyama wakali kuvamia makazi ya watu.


"katika wilaya hii pia tuna programu ya kutoa  ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Kaya masikini lakini pia kutoa mafunzo ya wanafunzi wa shule za sekondari kujitambua na kujua masuala ya uhifadhi na Utalii"alisema.


MWISHO.

No comments: