GOD MWANGA ATENGENEZA BARABARA 23 KWA GHARAMA ZAKE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 18 January 2026

GOD MWANGA ATENGENEZA BARABARA 23 KWA GHARAMA ZAKE

 


Na Mwandishi wetu, Moshi


maipacarusha20@gmail.com


MCHIMBAJI maarufu wa madini mbalimbali nchini God Mwanga amejitolea na kufanikisha ujenzi wa barabara tofauti 23 katika eneo la Mwika Kirueni, Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro.


Mchungaji mstaafu John Mlay ameyasema hayo wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa 2026 zilizofanyika nyumbani kwa ukoo wa mzee Mathayo Mwanga katika eneo la Mwika Kirueni.


Mchungaji Mlay ameeleza kwamba Mkurugenzi wa kampuni ya God Charity, Godlisten Mwanga amekuwa baraka kwa wakazi wa eneo hilo na kutengeneza barabara hizo kwa gharama zake mwenyewe.


"Huyu baba amefanya jambo jema kwani ametumia magari na mitambo yake binafsi na kutengeneza barabara 23 kwa gharama zake mwenyewe," amesema Mchungaji Mlay.


Amesema barabara hizo 23 zilikuwa na changamoto ya ubovu na hasa wakati mvua zikinyesha zinapitika kwa shida mno ila baada ya kutengenezwa hivi sasa hazina shida.


"Hivi sasa barabara hizi zinapitika kwa urahisi mno baada ya God Mwanga kufanya kazi hiyo kubwa ya kuzitengeneza na kunufaisha jamii inayoishi maeneo haya," amesema mchungaji Mlay.


Akizungumza kwenye sherehe hizo Mkurugenzi wa kampuni ya God Charity, Godlisten Mwanga amemshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka 2025 salama na kuingia mwaka mpya wa 2026.


"Pia namshukuru baba yetu mzee Mathayo Mwanga mwenye umri wa miaka 96 amekuwa nguzo ya familia kwani ametusimamia vyema kwa upendo, umoja na mshikamano," amesema Mwanga.


Mkazi wa Mwika Kirueni, Christopher Aloyce amempongeza God Mwanga kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hizo na kuwaondolea kero ya ubovu hasa nyakati mvua zikinyesha.


Aloyce amesema awali barabara hizo zilikuwa zinapitika kwa shida na wagonjwa waliokuwa wanabebwa na magari wanaopelekwa hospitali hasa wanawake wajawazito walikuwa wanapata shida mno.


MWISHO

No comments: