Oparesheni kuwakamata wachimbaji haramu yanukia - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 26 January 2026

Oparesheni kuwakamata wachimbaji haramu yanukia






Burhani Yakub,Muheza.


maipacarusha20@gmail.com

Vyombo vya ulinzi Wilayani hapa vinatarajia kuendesha oparesheni ya kuwasaka watu wachimbaji haramu wa madini wanaoendesha shughuli hizo katika vyanzo vya maji vya vilivyopo Tarafa za Amani na Bwembwera.


Oparesheni hiyo inalazimika kuendeshwa kufuatia wimbi la uharibifu wa vyanzo vya maji vilivyo chini ya Bodi ya bonde la Pangani kushamili baada ya kuibuka upya kwa wachimbaji haramu wa dhahabu katika vijiji vilivyopo kwenye milima ya Usambara Mashariki Wilayani hapa.


Mkuu wa Wilaya ya Muheza,Ayubu Sababili ametoa taarifa hiyo leo wakati akifungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya watumiamaji mto Kihuhwi (Juwamakihu) uliifanyika mjini hapa.


Amesema oparesheni hiyo atakayoiongoza itashirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama,wadau wengine wakiwamo Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Tanga (Tanga -Uwasa),Ruwasa,ofisi ya Afisa madini,Bodi ya bonde la Pangani,TFS pamoja na wananchi wanaoishi katika vijiji 16 vinavyozunguka vyanzo hivyo.


"Siwezi kutaja siku tutakayoanza oparesheni hii ambayo itakuwa endelevu lakini nieleze tu kuwa wote wanaofanya uharibifu wa vyanzo vya maji ya bonde la Pangani watambue kuwa tutawakamata haraka sana na kudhibiti uharibifu"amesema Sebabili.


Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali haiwezi kuvumilia uharibifu unaofanyika katika vyanzo vya maji kwa kuwa madhara yake ni makubwa.


"Tukiwaacha hawa waharibifu kuendeleza uchimbaji wa madini katika vyanzo vya maji madhara yake ni makubwa kwani maji yatakauka na wakazi wa Wilaya za Tanga,Muheza,Pangani,Mkinga na maeneo mengine yanayotegemea kusambaziwa maji kupitia vyanzo hivi watakosa kabisa huduma ya Maji safi na salama"amesema Sebabili.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiamaji wa mto Kihuhwi,(Juwamakih),Mohamed Msumari amesema wachimbaji haramu wa dhahabu wamerejea Kwa kasi kubwa katika vijiji sita vilivyopo kwenye vyanzo vya maji na hivyo kuwepo na hatari ya kukauka vyanzo hivyo.


Amevitaja vijiji anbavyo vimevamiwa na wachimbaji haramu wa dhahabu kuwa ni Bombani,Kwaisaka,Nkumba Kibanda,Zeneti,Mashewa na Msoweto.


Afisa Kidakio cha mto Zigi na Umba Tanga,Yusuph Mahenge amesema vyanzo hivyo vinatumika kusambaza maji safi na salama katika Wilaya za Tanga Muheza Pangani na Mkinga na kwamba iwapo vitaharibiwa wakazi wa eneo Hilo watakosa huduma hiyo.


"Uchimbaji wa madini katika vyanzo vya maji ni hatari kubwa kwa sababu ni uharibifu wa ikolojia ya maji ambayo yanatumiwa na binadamu,mimea na viumbe wengine hai,hakuna kampuni yoyote inayoruhusiwa kuchimba madini kwenye vyanzo vya maji...tunashukuru kusikia taarifa ya kuendeshwa kwa oparesheni"amesema Mahenge.


Hata hivyo Herieth Yohana kutoka kijiji Cha Kimbo Wilayani Muheza amesema changamoto wanaokumbana nazo katika kuwadhibiti wachimbaji haramu ni kwamba wanapofikishwa kwenye vyombo vya dola huachiwa na kutushia maisha ya waliowakamata.


"Tukiwakamata tukiwapeleka vyombo vya dola unakuta wanaachiwa haraka na wakirudi kijijini wanatishia maisha yetu...ni matarajio yetu kwamba oparesheni hiyo itawadhibiti wachimbaji haramu"amesema Herieth.


MWISHO

No comments: