![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima |
![]() |
| Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa CAMFED Anna Sawaki |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MRADI wa elimu ya Stadi za Maisha unaotekelezwa na CAMFED Tanzania umetakiwa kupokelewa, kusimamia na kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu ili watoto hususani wasichana wanufaike kieleimu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Riziki Shemdoe alitoa agizo hilo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima, wakati wa mkutano mkuu wa kitaifa wa wadau CAMFERD Tanzania uliofanyika mkoani Morogoro.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya, idara na taasisi zote nchini kuupokea, kuusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa Mradi huo unaotekelezwa kwa karibu zaidi.
Kaulimbiu “Wekeza Elimu kwa Maendeleo Endelevu”.
Shemdoe alisema mradi huo unaotekelezwa katika mikoa 10 nchini kwa ushirikiano kati ya Serikali na CAMFED umeanza kuonesha matokeo chanya, hivyo ni wajibu wa mikoa yote kuhakikisha unatekelezwa ipasavyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa CAMFED Anna Sawaki, alisema CAMFERD TANZANIA kwa kushirikiana na Serikali imeendelea kutekeleza miradi yake katika Halmashauri na Wilaya 35 katika mikoa 10, kwa lengo la kuboresha upatikanaji,ubora na usawa wa elimu.
Sawaki alisema kuwa tangu kuanzishwa kwake CAMFED Tanzania umesaidia wanafunzi 183,629 kwa kupata ufadhili wa elimu ya sekondari,na wanafunzi 38,928 walifikiwa kwa Mwaka 2025 huku ngazi ya Chuo wakiwa wanafunzi 4,645 na wasichana 225 wakipata Elimu ya ufundi,diploma 256 na 1,257 ni wa elimu ya chuo kikuu.
Alisema katika mwaka 2025 CAMFED imefanikiwa kuwafikia watoto takribani 39,000 katika ngazi ya elimu ya sekondari kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Sita..
Aidha, taasisi hiyo pamoja na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo pia limesaidia zaidi ya wasichana 8,000 kwa kuwapatia mikopo midogo na mikubwa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Akizungumzia Mradi wa Elimu ya Stadi za Maisha, Sawaki alisema kuwa mwaka 2025 CAMFED ilipata ithibati ya matumizi ya kitabu cha stadi za maisha ( Dunia yangu bora ), ambapo kuanzia mwaka wa masomo 2026, kitabu hicho kitaanza kutumika rasmi katika shule za sekondari ndani ya Halmashauri 76, kutoka Halmashauri 35 zilizokuwa zinatekeleza miradi ya CAMFED.
"Lengo la elimu ya stadi za maisha ni kuwasaidia wanafunzi kujitambua, kuweka malengo na kuwawezesha kufikia ndoto zao,"alisema.
Mmoja wa wanufaika wa miradi ya CAMFED, Eva John kutoka Wilaya ya Bagamoyo, alisema mkopo alioupata kutoka CAMFED ulimwezesha kununua vifaa vya kusindika matunda na mbogamboga na kuanzisha kiwanda kidogo.
“Kwa sasa nimekuwa mjasiriamali ninayejihusisha na usindikaji na nina kiwanda kidogo kinachosindika matunda kwa kuyakausha na kuyageuza kuwa unga,"alisema.
Alisema yeye kama msichana mwenye malengo, atahakikisha anawainua wasichana wengine katika jamii yake kwa kuongeza thamani ya mazao na kutatua changamoto wanazokutana nazo.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment