Na Mwandishi Wetu, Moshi
maipacarusha20@gmail.com
Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amekabidhiwa hati ya pongezi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Moshi Vijijini kwa niaba ya Serikali, kufuatia uwasilishaji wake wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa hiyo, DC Mnzava aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Halmashauri ya Moshi Vijijini imepokea jumla ya Sh bilioni 47.9 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 2.4 ni mapato ya ndani ya halmashauri, huku Sh bilioni 44.6 zikitoka Serikali Kuu.
“Katika kipindi hiki cha Julai hadi Desemba 2025, Halmashauri ilikuwa tayari imepokea jumla ya Sh bilioni 47.9, ambapo Sh bilioni 2.4 ni mapato ya ndani na Sh bilioni 44.6 ni fedha kutoka Serikali Kuu,” amesema DC Mnzava.
Katika sekta ya afya, amesema halmashauri imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, zahanati nne pamoja na ukarabati wa zahanati moja, ambapo jumla ya Sh bilioni 1.9 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wake.
Aidha, katika sekta ya nishati, amesema serikali jumla ya Sh bilioni 6.1 zimetumika kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 25 kati ya 45 vilivyokuwa vimesalia.
DC Mnzava amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia wilaya hiyo fedha za maendeleo na kusisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa rasilimali hizo.
“Tumshukuru Rais wetu kwa kuendelea kutuletea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya yetu. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia fedha zote zilizoletwa ili zitekeleze malengo yaliyokusudiwa,” amesema.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment