![]() |
| Meneja Tanesco Mkoa wa Pwani kusini.Eng.Anita Marco akikabidhi Jiko kwa mnufaika wa Jiko aina ya Pressure Cooker |
Na Lilian Kasenene,Pwani
maipacarusha20@gmail.com
SHIRIKA la umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani kusini, limeendelea na kampeni ya uelimishaji na ukopeshaji wa majiko ya kisasa yenye teknolojia za kutumia umeme kidogo kwa wananchi wa Wilaya za Mafia, Kibiti, Ikwiriri, Pamoja, na Mkuranga.
Meneja wa Tanesco mkoa wa Pwani kusini Mhandisi Anita Marco akikabidhi majiko hayo alisema lengo ni kuhimiza na hakikisha kila mwananchi anatumia majiko hayo ya gharama nafuu.
"Tanesco inakopesha majiko haya na unalipa kidogo kidogo kupitia mfumo wa Luku,"alisema meneja huyo.
Majiko haya ya kisasa, yenye nishati safi na ufanisi mkubwa, yanasaidia kuokoa muda na gharama.
Mhandisi Anita Marco pia alisema kuwa majiko haya hutumia nishati kidogo ambayo ni salama, husaidia kuhifadhi mazingira, na kuwezesha jamii kutumia rasilimali kwa ufanisi.
Majiko hayo ni aina ya Pressure Cooker yanayotumika umeme mdogo yakiwa na teknolojia ya IoT kutoka Sayari Safi na washirika wa Up Energy.
Alisema wananchi wanaweza kupima na kudhibiti matumizi ya nishati kwa urahisi na Wateja 14 tayari wamepata faida kupitia mkopo wa malipo ya luku kuanzia Tsh 12,500 kwa mwezi, sawa na Tsh 150,000 kwa mwaka.
Aidha Tanesco inahimiza matumizi ya nishati safi, nafuu, na rahisi, ikisaidia wananchi kuokoa pesa, Muda, na rasilimali, huku wakilinda mazingira ambapo kwa Pwani Kusini, nishati safi ni suluhisho la kila siku linaloongeza ufanisi, usalama, na uhifadhi wa rasilimali.
Majiko ya umeme yanayotumia teknolojia ya IoT (Internet of Things) yameundwa kupunguza matumizi ya nishati, hivyo kuokoa gharama na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi kwa watu wa kipato cha chini.
Pia yanapunguza matumizi makubwa ya umeme ikilinganishwa na majiko ya zamani, huku yakilenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment