KITABU CHA DUNIA YANGU BORA CHAPATA ITHIBATI,CAMFED YAFIKIA HALMASHAURI 76 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 18 February 2026

KITABU CHA DUNIA YANGU BORA CHAPATA ITHIBATI,CAMFED YAFIKIA HALMASHAURI 76





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com

SERIKALI imekipatia rasmi ithibati kitabu cha Dunia yangu Bora ambacho kitaanza kutumia sasa katika shule za sekondari zilizopo kwenye halmashauri za wilaya 76 ndani ya Mikoa 10 nchini.

Wanafunzi hao wataanza kufundishwa stadi za maisha kupitia kitabu hicho.



Mkuu wa Idara ya Miradi kutoka shirika la Campaign For Women Education(CAMFED) walioasisi kitabu hicho Dominica Lyambo alisema awali kabla ya kupewa ithibati walitumia kukifundisha kwa halmashauri 35 lakini sasa wanaongeza halmashauri 41 zaidi ili kufikisha halmashauri 76.

Alisema lengo kubwa la kitabu hicho ama stadi za maisha zilizomo ni kuwafanya wanafunzi wa Sekondari wanajitambua kwanini wako shuleni,shule zinaongeza mahudhurio, kiwango cha ufaulu kitaongezeka,

"Ni stadi za maisha, zinaelezea kwanini mwanafunzi uko shule, kwanini unatakiwa usome, kuna changamoto gani zipo kwenye jamii ambazo wewe kama mwanafunzi huwezi kuzitatua, lakini namna gani unakabiliana na hizo changamoto ili kufikia ndoto zako za baadaye,"alisema Lyambo.

Alisema mpango wa CAMFED ni kuhakikisha ifikapo 2030, wanazifikia asilimia 85 ya halmashauri zote za wilaya zilizopo nchini kwenye mikoa 26 badala ya 10 waliyoifikia sasa.

"Na cha kuzingatia Kitabu hiki hawaendi kutumia wasichana peke yao,wanatumia Wanafunzi wavulana kwa wasichana, na mwezeshaji atakavyokwenda kuwezesha shuleni anawezesha Wanafunzi wote kwa kidato cha kwanza na cha pili, na program hii itakuwa endelevu"alisisitiza mkuu huyo wa Idara ya miradi wa CAMFED.

Aliongeza kuwa vijana wawezeshaji wa program hiyo watanufaika na program hiyo kwa kuwa mfano wa kuigwa (role models) kwenye jamii zao, wakiwa eneo la shule watakutana na fursa mbalimbali kwani watasaidiana na halmashauri  za wilaya kwani wapo kwenye umri wa kutafuta kazi na maisha kutumia fursa za halmashauri za maeneo yao.

Akasema kila halmashauri imetoa Walimu kati ya wawili hadi wanne ili kujengewa uwezo ambao watakwenda kufundisha wawezeshaji wengine watakaowafundisha wengine ngazi za shule za Sekondari ili wakafundishe Wanafunzi madarasani.

Kuhusu tofauti ya kitabu hicho na vingine, Alisema kitabu hicho ni cha kipekee tofauti na vya masomo na kinamgusa binadamu yeyote,wa umri au taaluma yeyote, kikielezea ustawi wa mtu,mahitaji ya msingi na matakwa, uwezo wa mtu wa ndani, kumjenga mwajiri kuwa mzuri katika stadi za kusimamia wengine, namna Wanafunzi wanavyoweza kuhimili changamoto na mihemko yao na kufaulu vizuri.



Afisa mwandamizi ofisi ya Kamishna wa Elimu,Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Fredy Nyandoro akataja maudhui yaliyo kwenye kitabu hicho kuwa ni stadi za maisha na kimepewa ithibati kama kitabu cha ziada na kitasambaza mahitaji yaliyopo kwenye jamii kutokana  na masomo wanayofundishwa ikiwemo historia ya Tanzania na maadili.

"Vijana wengi katika Dunia ya sasa wanakabiliwa na changamoto ya kupotoka kwa maadili, na maudhui ya kitabu hiki yanamlenga kijana wa kitanzania, mwanafunzi wa rika balehe kuwa mwaminifu, mwadilifu, kujituma, kujali wengine, kuwa na upendo, kutenda matendo mema ya utu, kutunza mazingira, Dunia yangu Bora inalenga kumfanya kijana apende Dunia, ayapende mazingira, ayaboreshe, ayahifadhi akijua kuna jamii inaishi kwenye haya mazingira,"alisema

Akasema kitabu hicho kina visa mkasa vingi  na hadithi ambazo zinaangazia namna ya kutatua changamoto ambazo kijana anakutana nazo, namna ya kufanya mazingira ikiwemo watu,marafiki na Jamii inayowazunguka katika kutatua changamoto za maisha.

"Kitabu kinafundisha hakuna kukata tamaa kwenye maisha,unpokutana na changamoto ujue namna ya kushirikisha wazazi, marafiki au ndugu unayemwamini kutatua, na changamoto zilizopo kwenye jamii hazitatuliwi na mtu mmoja, lazima kuwe na ushirikishwaji wa mawazo ya watu tofauti,kitabu pia kinampa nafasi mtoto wa kike mbinu za namna ya kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu wao,"aliongeza.

Akizungumza na walimu hao, Mwakilishi wa Kamishna wa elimu nchini Dk Gladness Kirei alizitaka halmashauri 76 kuwa na mpango kazi wa kuendesha elimu ya stadi za maisha mashuleni na kutaka somo hilo lisichukuliwe kama somo la ziada kama kilivyo kitabu husika.

Akawaagiza maafisa elimu kata kufuatilia maendeleo ya program hiyo kwa kukusanya mahudhurio na kufanya tathmini ya ufundishaji ili kuona wale wanaofanya vizuri au kulega lega.

Akataka shule kuwashirikisha wazazi kuhusu elimu ya stadi za maisha na kuandaa mikutano au semina zenye lengo la kuwajengea uwezo wazazi juu ya mradi huo wa stadi za maisha.

"Mafanikio ya mradi huu hayatapimwa kwa idadi ya vitabu vilivyotolewa, au walimu wangapi wamefikiwa, bali yatapimwa kwa mabadiliko ya vijana, mahudhurio yao shuleni, kupungua kwa mimba za utotoni pamoja na kiwango cha ufaulu,"alisema Dk Kirei.

Mwisho.

No comments: