MAREMA WAOMBA GETI LA TANZANITE KUWA WAZI SAA 24 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 13 February 2026

MAREMA WAOMBA GETI LA TANZANITE KUWA WAZI SAA 24

 


Na Mwandishi wetu, Mirerani 


maipacarusha20@gmail.com 


WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba serikali kuruhusu lango la kuingia na kutoka ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite kuwa wazi saa 24 ili shughuli zao zifanyike vyema.


Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi ameyasema hayo mbele ya mkuu wa moa huo Queen Sendiga kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika mji mdogo wa Mirerani. 


Mnyawi ameeleza kwamba changamoto ya lango la kuingia na kutoka ndani ya ukuta kufungwa saa 5 usiku inawakwaza wachimbaji madini ya Tanzanite.


Amesema endapo lango hilo likiwa wazi saa 24 kwa siku itakuwa vyema kwani shughuli za kiuchumi zitakuwa zimeboreshwa zaidi.


"Tunavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya ukuta kwani wanafanya kazi nzuri ila wachimbaji wangepewa fursa ya lango hilo kuwa wazi saa 24 itakuwa bora zaidi kwao," amesema Mnyawi.


Amesema endapo suala hilo litapata kibali itaongeza pato la wachimbaji madini na Taifa kwa ujumla kwani uzalishaji utakuwa juu zaidi. 


Hata hivyo, RC Sendiga amemuagiza DC Simanjiro, Fakii Lulandana kukaa na kamati yake ya usalama ya ukuta huo na kulijadili kwani lipo ndani ya uwezo wao.


"DC Simanjiro hawa wachimbaji madini ya Tanzanite ni wadau wenu na hili lipo ndani ya uwezo wenu, mngekaa kamati yenu ya usalama ya ukuta na kuangalia namna ya kufanya," amesema RC Sendiga.


Pia, amewapongeza MAREMA kwa kufanya kikao chao cha mwaka kwa amani na kuzungumza mambo yao na kujipanga kwa mwaka huu mpya wa 2026.


Ofisa madini mkazi Manyara, RMO Godfrey Nyanda amesema wamekuwa na Ushirikiano mkubwa na wachimbaji hao kupitia mkutano huo mkuu wa siku mbili kwani wamesikiliza changamoto na mafanikio yao.


Nyanda ameeleza kwamba hata katika uchangiaji wa makusanyo ya mwaka katika eneo lao wachimbaji wadogo wamechangia Sh500 milioni.


"Tunakukaribisha katika kikao hiki cha wachimbaji madini, tunasubiria kutekeleza maelekezo yako kwetu sisi wasimamizi wa sekta ya madini na wachimbaji kwa ujumla," amesema Nyanda.


Mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Sadiki Mneney amesema suala la lango la kuingia na kutoka ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite kuwa wazi saa 24 itachochea zaidi uchumi wa eneo hilo. 


"Maeneo mengi yanafanya kazi kwa saa 24 hata soko la Kariakoo linafanya kazi usiku kucha hivyo na lango hilo liwe wazi saa zote kuliko hivi sasa linafungwa saa 5 usiku," amesema. 


Amesema hata mtu akipata ajali usiku wa manane akiwa mgodini anashindwa kupata matibabu thabiti kwani ndani ya ukuta hakuna zahanati wala kituo cha afya. 


MWISHO

No comments: