MISA - TAN, EWURA YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI KUANDIKA HABARI ZA NISHATI NA MAJI KWA TIJA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 27 February 2026

MISA - TAN, EWURA YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI KUANDIKA HABARI ZA NISHATI NA MAJI KWA TIJA









Na Andrea Ngobole, maipac


maipacarusha20@gmail.com 


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendesha warsha ya tathmini ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kwa lengo la kuimarisha uelewa wao kuhusu majukumu, mipaka ya kisheria na utendaji wa mamlaka hiyo katika sekta za nishati na maji nchini.


Warsha hiyo imefanyika leo Februari 27, 2026 jijini Dar es Salaam, katika Ukumbi wa SeaShells Hotel, ikiwakutanisha wahariri na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari.


Lengo kuu lilikuwa kupima mafanikio ya mafunzo yaliyotolewa awali na kuweka mikakati mipya ya kuboresha ushirikiano kati ya EWURA na vyombo vya habari.
Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Long’idu akifungua warsha ya tathmini ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kwenye kuifahamu EWURA na majukumu yake

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Long’idu, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha umma kuhusu majukumu ya EWURA, ikiwemo udhibiti wa bei, utoaji leseni, na usimamizi wa ubora wa huduma za nishati na maji.


Amesema kuwa kuwajengea uwezo waandishi ni sehemu ya mkakati wa EWURA wa kuhakikisha taarifa zinazotolewa kwa umma zina usahihi, uwiano na zinaakisi hali halisi ya majukumu ya mamlaka hiyo. “Mnapoelewa vizuri tunachokisimamia, mnakuwa daraja sahihi kati ya EWURA na wananchi,” amesisitiza.

Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, akitoa tathmini ya habari zilizoripotiwa na wanahabari kuhusu EWURA kwa kipindi cha miezi sita

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema warsha hiyo ni muendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili, akibainisha kuwa mafunzo yaliyopita yalizaa matunda ambapo jumla ya habari 103 zilichapishwa katika kipindi cha miezi sita zikihusu shughuli za EWURA.


Ameongeza kuwa lengo la warsha za tathmini ni kuibua waandishi mahiri (“champions”) watakaoweza kuandika kwa weledi, kuzingatia maadili ya taaluma na kusaidia kujenga uwajibikaji katika sekta ya nishati na maji kuwa na mtazamo mpya kuongeza tija kwa wananchi.

Soko ametoa wito kwa waandishi kuendelea kuandika kwa weledi, kufanya uchambuzi wa kina na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi zinazochochea uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu ya Taifa.

Akiwasilisha mada katika warsha hiyo Wilfred Mwakalosi, meneja kitengo cha mawasiliano kwa umma (EWURA) Amesema uongozi mzuri unaowajibika kwa umma umeweza kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Gesi majumbani, mafuta na umeme kwa upande wa nishati pia watoa huduma wa maji wanatia elimu kwa wateja wao.
Marko maduhu mwandishi wa habari wa Nipashe Shinyanga akisikiliza kwa makini mada zinazowasilisha

No comments: