TAKUKURU MOROGORO YAOKOA MILIONI 100 ULANGA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 27 February 2026

TAKUKURU MOROGORO YAOKOA MILIONI 100 ULANGA

 

Kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Morogoro Dk Herry Mwankusye

Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Morogoro imefanikiwa kuokoa kiasi cha sh milioni 100 zilizokuwa zimetengwa na Halmashauri ya Ulanga kwa ruzuku ya mbegu na miche.


Fedha hizo zilizookolewa ni  za kuanzia kipindi cha Oktoba Hadi Desemba, 2025.


Kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Morogoro Dk Herry Mwankusye alieleza hayo wakati alitoa taarifa ya miezi mitatu inayohusu  mafanikio ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa vyombo vya habari.


Akimwakilisha mkuu wa Takukuru mkoa huo, Mwankusye alisema kupitia taarifa ya wadau, Takukuru Wilaya ya Ulanga ilifanya uchambuzi wa mfumo wa manunizi na ugawaji ruzuku ili kubaini mianya ya Rushwa na mapungufu mbalimbali yaliyolalamikiwa.


"Katika malalamiko haya ambayo yalikuwa yanahatarisha matumizi ya fedha kiasi hicho zilizotengwa kwa ajili ya ruzuku ya mbegu na miche na kubaini mapungufu,"alisema.


Baada ya kubainika kwa mapungufu yaliyokuwa yanahatarisha  matumizi yasiyofaa ya fedha hiyo Takukuru ilitoa mapendekezo iliyowakutanisha wadau wa kilimo, ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo kwa kupanda ratiba za manunuzi, kushirikisha wakulima na  AMCOS ili kubaini mahitaji halisi ya mbegu na kutumia malipo ya kielektroniki na kuandaa rejista ya walionufaika,ili kuimarisha uwajibikaji,uwazi,imani ya wakulima kwa Halmashauri na AMCOS kuongezeka na kuhakikisha Kila sh ya umma inaleta matokeo.


Aidha alisema katika hicho  Takukuru ilisaidia fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi  yenye thamani ya sh bilioni 1 iliyokuwa na mapungufu kutekeleza kulingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa.


"Kwa ujumla tulifuatilia matumizi zaidi ya bilioni 4 kwenye utekelezaji wa miradi ya Maendeleo 13 katika sekta ya Elimu na afya,"alisema.


Katika uchunguzi alisema walipokea malalamiko 71 kati ya hayo malalamiko 51 yalihusu vitendo vya Rushwa katika hatua mbalimbali, ambapo malalamiko 20 hayakuhusu rushwa na walalamikaji wake walishauriwa na mengine kupelekwa idara husika.


Kaimu huyo wa Takukuru alitaja kesi mpya katika kipindi hicho kuwa ni 5, zilizoamuliwa ni kesi 9, walizoshinda 5, kesi zilizoondolewa ni nne na kesi zinazoendelea mahakamani ni kesi 4.


Mwankusye alisema katika kushinda kesi hizo watuhumiwa walilipa faini, licha ya kulipa faini wapo waliorejesha fedha za umma katika utaratibu wa makubaliano wa kukiri kosa.


Alitaja Wilaya zilizoongoza katika kesi za Rushwa ni Halmashauri Kilombero, Kilosa na ofisi ya mkoa


Pia alisema Takukuru unaendelea kutoa Elimu kwa wanafunzi, wananchi na watumishi wa umma kuhusu athari za Rushwa na umuhimu wa kujiepusha na vitendo hivyo ambapo wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.


Mwisho..

No comments: