Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kuongeza nguvu katika usimamizi mazao ya nyuki na kufikia uzalishaji wa asali tani 50,000 kwa mwaka ambazo zitasafirishwa nje ya nchi.
Kwa sasa uzalishwaji wa asali na unaosafirishwa nje ni tani 9 kwa mwaka.
Naibu Waziri wa Maliasili na utalii Hamad Hassan Chande aliyasema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mkutano mkuu wa nne wa mwaka wa makamanda wa Kanda Saba wa wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS,wahifadhi wakuu wa Wilaya, wa mashamba,hifadhi wa Misitu ya Mazingira asilia na vituo vya Mali kale.
Naibu Waziri huyo pia aliwaagiza TFS kuendelea kufanya utafiti zaidi ili zao hilo la nyuki liweze kufika ulimwenguni.
"Kwenye mazao ya nyuki niwapongeze sana TFS kwa usimamizi wenu mzuri unaofanya tuweze kupata asali bora ulimwenguni lakini niwape rai endeleeni kufanya utafiti kwenye mazao mengine ya nyuki ikiwemo sumu ya nyuki ambayo inahitajika sana ulimwenguni, vumbi la nyuki na na," amesema Chande.
Aidha Naibu waziri huyo aliwataka TFS kuendelea kutoa elimu Kwa jamii inayowazunguka hasa katika matumizi ya mizinga ya kisasa ya kufugia nyuki.
Katika hatua nyingine aliuagiza uongozi wa TFS kuwapa fursa askari na makamanda wao za kwenda kusoma ili waweze kupata weledi, waweze kuongeza maslahi yao lakini pia waweze kutumia elimu kufanyakazi Kwa maslahi ya TFS.
Katika utendaji kazi wa kila siku Naibu waziri huyo aliwataka makamanda, maafisa na wafanyakazi wa TFS kumuogopa na kumtanguliza mungu, kuwa na subira katika mipango yao mbalimbali ya kimaendeleo, kujenga imani kwa waliowaamini na kuamini malipo mbele za mungu ya chochote watakachokifanya.
Akitoa taarifa ya utendaji wa TFS kamishana wa uhifadhi Profesa Dosantos Silayo alisema mkutano huo ni mahususi na ni mbadala wa vikao vya mabaraza ya wafanyakazi TFS ambavyo viliondolewa baada ya TFS kubadilishwa mfumo kutoka kwenye mfumo wa kiraia kwenda kwenye mfumo wa kijeshi.
"Mwaka 2018 TFS iliwekwa kwenye mfumo wa kijeshi na hapo ndio tukatafuta jukwaa la kuwakutanisha askari wetu Ili waweze kuelekza changamoto, mafanikio na kutoa maoninya namna jeshi liweze kusonga mbele,"alisema Prof. Silayo.
Alisema mkutano huo pia utatumika kutoa mafunzo mahususi kwa askari na kwamba wataalamu mbalimbali wabobezi wamealikwa kutoa mada kulingana na mahitaji.
Baadhi ya mada zitakazofundishwa kwenye mkutano huo ni pamoja na masuala ya afya ya akili na magonjwa yasiyoambukiza, namna ya kujitambua wao wenyewe na wanaowaongoza lakini pia makamanda hao watafanya bonanza la michezo mbalimbali.
Kuhusu mafanikio Prof. Silayo alisema TFS umeweza kujenga majengo mapya 138 yakiwemo majengo ya ofisi na vituo vya ulinzi wa misitu huku akieleza changamoto ametaja migogoro ya mipaka ya hifadhi na vijiji.
Mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu wizara ya maliasili na utalii Bernard Marceline aliwapongeza watumishi wa TFS kwa kufanyakazi Kwa bidii na uadikifu mkubwa.
"Nipo pale wizarani kwa miaka mitatu sasa miongoni kwa taasisi ninazofanyanazo kazi vizuri ni pamoja na TFS, sijawahi kupokea malalamiko kutoka TFS, kiukweli mnachapa kazi,"alisema Marceline.
Naye mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TFS Luteni mstaafu Chiku Galawa alisema Rais Samia Suluhu Hassan alifanyakazi kubwa kuitangaza nchi kupitia Royal tour huku lengo ni kufikia watalii milioni 8 ifikapo 2030.
Mwisho.





No comments:
Post a Comment