NEMC YATEKETEZA TANI 20 ZA VIFUNGASHIO NA VIBEBEO VISIVYOKIDHI VIWANGO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 17 February 2026

NEMC YATEKETEZA TANI 20 ZA VIFUNGASHIO NA VIBEBEO VISIVYOKIDHI VIWANGO

 



Na mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeendesha zoezi la uteketezaji wa vifungashio na vibebeo vilivyokuwa vikisambazwa katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa hususani mkoa wa Mwanza.


Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 17 Februari 2026, kupitia Mitambo ya uteketezaji ambayo ni rafiki wa mazingira, iliyopo katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote Mkoani Mtwara.


Meneja wa NEMC Kanda ya Kusini, Gift Ngowo amesema sehemu ya shehea hiyo iliyoteketezwa ni mifuko ya plastiki iliyokosa ubora, ambayo ilikamatwa kwa ushirikiano na mamlaka zingine pamoja na Jeshi la polisi.


Ametaja kiasi cha vifungashio na vibebeo hivyo kuwa ni katoni 1,699 sawa na Tani 20, na kusisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu likiwa linalenga kuhakikisha kuwa mifuko hiyo haiendi sokoni kwa sababu imekosa ubora.


Ametoa rai kwa wafanyabishara nchini kuacha  kuzalisha,kusambaza na kuiuza vifungashio na vibebeo visivyoruhusiwa, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.


Pia ametoa rai kwa wananchi kutambua madhara ya matumizi ya mifuko hii kwa Afya ya binadamu,viumbe hai na mazingira, na wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi sambamba na wafanyabiashara kuwa  NEMC itachukua hatua za kisheria ili kuendelea kudhibiti hali hiyo.


Kwa upande wake Samuel Nyasani, Afisa Mazingira mwandamizi Nemc Kanda ya Ziwa, amesema lengo la zoezi hilo pia ni  kutoa ujumbe kwa wafanyabiashara ambao sio waaminifu.


Amesema kuwa kuna vifungashio vinavyoruhusiwa kisheria vikiwepo vinavyotumika  kwenye bidhaa za viwandani,mahospitalini na kwenye bidhaa za kilimo, lakini kumekuwa na watu wasio waaminifu ambao wanakiuka sheria na kanuni zilizowekwa.

No comments: