Mwandishi wetu,Meatu
maipacarusha@gmail.com
Meatu. Serikali wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu, imewataka wafugaji katika wilaya hiyo, kuacha kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi za Utalii na imetoa mbegu za kiasi cha kilo 1900 kwa vijiji 21 kwa ajili ya Malisho.
Wilaya ya Meatu ni miongoni mwa wilaya za kimkakati nchini, katika kuendeleza uhifadhi na Utalii, ikiwa inapakana na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba la Maswa na hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Makao.
Akizungumza na waandishi wa Habari, baada ya ziara katika maeneo mbali mbali ya wilaya hiyo, kukagua shughuli za Maendeleo, Mkuu wa wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura alisema, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo maeneo yaliyotengwa kwa uhifadhi jambo ambalo limepigwa marufuku.
Ngatumbura alisema katika eneo la Makao, ambapo kuna uwekezaji mkubwa wa Utalii wa picha na hoteli ya kitalii Mwiba na maeneo ya Jirani yaliyotengwa kwa Uhifadhi na Utalii kumekuwepo na baadhi ya wafugaji ambao wanavamia hasa nyakati za kiangazi.
“Tumezungumza na wafugaji na tumekubaliana wasiingize mifugo katika maeneo ya hifadhi na kwa kuwa kilio chao ni malisho basi Serikali imechukuwa hatua ya kuwasaidia kupata mbegu za majani kwa ajili ya malisho”alisema
Alisema wilaya hiyo, imetoa mbegu kiasi cha kilogramu 1900 kwa wafugaji 337 wa vijiji 21 katika wilaya hiyo na sasa wameanza kupanda ili kujihakikishia malisho ya mifugo ya Uhakika.
“ Mbegu hizi zikipandwa vizuri zinaweza kuzalishwa katika eneo la heka 190 na hivyo, kupunguza kabisa tatizo la malisho ya mifugo katika wilaya hiyo”alisema
Mkuu huyo wa wilaya alieleza wilaya hiyo, imejipanga kuongeza mapato katika sekta ya Utalii, kutokana na uwepo wa wawekezaji ambao wamewekeza katika wilaya hiyo, ikiwepo kampuni ya Mwiba Holding Ltd, ambayo inafanya utalii wa picha na hotel.
“Bado tuna maeneo kadhaa ya utalii na uhifadhi tunaalika wawekezaji wengine kuja Meatu,lakini pia watalii wa ndani na nje tunawaalika katika wilaya yetu ya Meatu”alisema
Diwani wa viti maalum, katika halmashauri ya Meatu, Zainabu Abdalah alisema sekta ya Utalii imekuwa na mchango mkubwa katika wilaya hiyo, kutokana na mazingira bora ya uwekezaji ambayo yamewekwa na Rais Samia Suluhu.
“Kikubwa katika wilaya yetu sasa ni kuyalinda maeneo yaliyohifadhiwa, wafugaji wetu wasivamie maeneo ya hifadhi ili tuendelee kunufaika na Utalii”alisema
Diwani Zuhura Chilumba wa halmashauri hiyo ya Meatu, alisema vijiji vingi vinanufaika na uwekezaji wa utalii, ikiwepo Kijiji cha Makao ambapo wanafunzi wanapata bure chakula kutoka kwa mwekezaji lakini pia huduma za afya, elimu na nyingine zimeboreshwa.
“Vijiji vya Makao, Mwanjoro,Sakasaka, Mbushi na vingine vinanufaika sana na fedha za Utalii na Uhifadhi sambamba na Kata katika maeneo hayo, sasa lazima tuendelee kutunza mazingira yetu”alisema
Katibu wa Jumuiya ya vijana ya CCM wilaya ya Meatu, Zamda Mohamed, alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu imetekeleza vizuri Ilani ya uchaguzi hasa katika sekta ya Utalii na Uhifadhi katika wilaya hiyo na sasa manufaa makubwa yanaonekana.
“Tumpongeze Rais Samia amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza Utalii ambao sisi Meatu tunaona matunda yake na sio hivyo tu bali pia wakulima wa Pamba wanapata masoko, miundombinu inaendelea kuboreshwa katika wilaya yetu”alisema
MWISHO.

No comments:
Post a Comment