OFISI YA DC SIMANJIRO WAFANYA UTALII WA NDANI TARANGIRE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 5 February 2026

OFISI YA DC SIMANJIRO WAFANYA UTALII WA NDANI TARANGIRE

 




 Na Mwandishi wetu, Simanjiro 


maipacarusha20@gmail.com


DC Simanjiro Mkoani Manyara, mwalimu Fakii Raphael Lulandala na DAS Simanjiro Warda Abeid Maulid na watumishi wa ofisi yao wametembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire kufanya utalii wa ndani, kujipongeza kwa kazi ya kutumikia jamii na kujipanga upya katika kuwatumikia wana Simanjiro kwa mwaka 2026.


Katika ziara hiyo wameona wanyamapori mbalimbali wakiwemo tembo, mbogo, simba, twiga, pundamilia, digidigi, fisi na nyumbu.


Akizungumza kwenye hifadhi hiyo DC Lulandala ameeleza kwamba kwa sababu amefikisha miaka miwili tangu aingie Simanjiro ameona ni vyema kusherehekea mwaka mpya wa 2026 akiwa na wafanyakazi wa ofisi yake.


"Natoa shukrani zangu za dhati kwenu kwani nikiwa mwakilishi wa Rais Samia Suluhu Hassan hapa Simanjiro mmekuwa msaada mkubwa kwangu kuhakikisha kazi zinafanyika vyema," amesema DC Lulandala.


Amesema kwa miaka miwili aliyoishi Simanjiro viongozi hao wamempa ushirikiano mkubwa katika Tarafa mbalimbali na kusogeza huduma kwa jamii kwa karibu mno.


"Tukaona tutembelee huku mbugani tutalii tuone wanyama, tule pamoja tufurahi, wenye kuogelea waogelee, wanaocheza muziki wafanye hivyo ili tukirudi makazini kwetu akili zifanye kazi upya katika kuwatumikia wana Simanjiro," amesema DC Lulandala.


DAS Simanjiro Warda Abeid Maulid amewapongeza watumishi hao wa ofisi ya DC Simanjiro kwa namna wanavyowajibika kwa jamii na kuwaasa wakirudi maofisi waendelee kufanya kazi kwa bidii.


"Kazi na utu, tunasonga mbele, Rais Samia Suluhu Hassan hoyee, DC wetu Lulandala hoyeee, watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro hoyeee, asanteni sana," amesema Warda.


Hata hivyo, maafisa Tarafa, makatibu muhtasi wa ofisi ya DC Simanjiro wamewapa zawadi ya mavazi DC Lulandala na DAS Warda ikiwa ni shukrani ya kuwasimamia vyema.


Afisa Tarafa ya Emboreet Beny Mwandalile amesema wamepata faraja katika ziara hiyo ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa wao kuburudika na Mkuu wa Wilaya hiyo kama familia moja.


 "Sisi ni wasaidizi wa ofisi ya mkuu wa wilaya ya Simanjiro katika Tarafa zetu, tunashukuru kwa mtoko huu wa utalii wa ndani kwani tumekuja kuburudika na kujipanga upya kutumikia jamii za maeneo yetu," amesema Mwandalile.


Afisa Tarafa Naberera Tumaini Sebastian amesema ziara hiyo umekuwa na mafunzo makubwa kwao kwani wameondoa uchovu na mawazo hasi na sasa wanakuja na nguvu mpya na mawazo chanja katika kutikiza majukumu yao.


 MWISHO

No comments: