Na mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
Zile fedha kiasi cha Sh. bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji biashara za vijana na wanawake sio ahadi tena, tayari Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeshazitoa na zimepokelewa.
Hatua hiyo, ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais Samia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, alipoahidi ndani ya siku 100 atakapoapishwa kuwa Rais, Serikali yake itatoa Sh. 200 bilioni kuwezesha biashara kwa vijana na wanawake.
Utekelezaji wa ahadi hiyo, unafuatana na ahadi nyingine kadhaa zilizotekelezwa, ikiwemo majaribio ya Bima ya Afya kwa Wote, ajira 7,000 kwa walimu wa sayansi na hesabu na kutozuiwa maiti kwa kushindwa gharama za matibabu katika hospitali za umma.
Makabidhiano ya mfano wa hundi wa kiasi hicho cha fedha yamefanyika jijini Dodoma leo, Alhamisi Februari 5, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar kwenda kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba amesema kiasi hicho ni nyongeza ya zile fedha ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ajili ya makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Ametaka masharti ya upatikanaji wa fedha hizo yawekwe wazi ili watu wasiendelee kuogopa, huku akizisisitiza taasisi za fedha kuhakikisha zinalegeza masharti ya uwezeshaji huo.

No comments:
Post a Comment