Na Mwandishi wetu, Mirerani.
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amekabidhi tuzo tatu kwa wachimbaji madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, ili kutambua mchango wao katika kufanikisha miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Sendiga akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) kilichofanyika kwa siku mbili mji mdogo wa Mirerani amewasihi wachimbaji kuikumbuka jamii.
Sendiga amekabidhi tuzo hizo kwa kampuni ya Franone mining LTD, God Charity LTD na Chusa mining LTD, kwa kutambua mchango wao katika kusaidia jamii kupitia miradi mbalimbali.
Amewataka wachimbaji wengine wa madini kuiga mfano huo kwa kuisaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.
"Tumeona wachimbaji hawa watatu kupitia kampuni zao wamefanya mambo makubwa kupitia CSR na kupatiwa tuzo ya kutambua mchango wao tunatarajia kuona CSR nyingine zaidi kwa jamii kwa mwaka huu mpya wa 2026," amesema.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amesema awali baadhi ya wamiliki wa migodi walikuwa wanatoa CSR bila kutoa taarifa na kuijulisha serikali juu ya miradi ya maendeleo iliyofanyika.
Mnyawi ameeleza kwamba kampuni ya God Charity imesaidia jamii katika mambo mengi mbalimbali ikiwemo kutengeneza miundombinu ya barabara na miradi ya maji, madarasa na nyumba za walimu.
Amesema kampuni ya Franone mining nayo imepatiwa tuzo kwa kuhudumia jamii katika miradi mbalimbali ikiwemo zahanati wanayojenga migodini itakayosaidia wachimbaji madini katika suala zima la huduma za afya.
Ameeleza kwamba kampuni ya Chusa mining LTD, pamoja na kusaidia jamii kwenye miradi mbalimbali wamepatiwa tuzo hiyo kwa kujenga wodi ya wanawake na watoto na ofisi kwenye kituo cha afya Mirerani.
"Tunawashukuru wachimbaji hao kwa CSR walizofanya hivyo ni funzo kwetu wachimbaji wengine tupate somo katika kusaidia jamii tusitoe kimya kimya ili serikali iwe na taarifa," amesema Mnyawi.
Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau amesema wachimbaji hao wa madini ya Tanzanite wamekuwa na moyo wa kufanya CSR kwa jamii ndiyo sababu wamekuwa wakipatiwa tuzo za heshima mara kwa mara.
"Tumekuwa tukiwapatia tuzo wachimbaji madini hawa mara kwa mara na kutambua mchango wao kutokana na wao kuwajibika kwa jamii wa maeneo haya," amesema Njau.
MWISHO

No comments:
Post a Comment