UN yampongeza Rais Samia kwa kuunda Tume ya Uchunguzi, yahimiza Maridhiano, Uponyaji Tanzania - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 7 February 2026

UN yampongeza Rais Samia kwa kuunda Tume ya Uchunguzi, yahimiza Maridhiano, Uponyaji Tanzania

 




Mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasilisha ujumbe maalum kwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, jijini Geneva, Uswisi, ikiwa ni hatua ya Tanzania kuendeleza ushiriki wake wa kidiplomasia na mifumo ya kimataifa ya haki za binadamu.


Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo umehusisha uwazi wa matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali kurejesha amani, kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kulinda haki za binadamu.


Akizungumza baada ya kuwasilisha ujumbe huo wa Dkt Samia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amemweleza Turk kuwa, baadhi ya simulizi zinazosambazwa kimataifa zimejaa upotoshaji na hazioneshi uhalisia wa hali ilivyo nchini. 


Amesisitiza kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti, ikiwemo kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, ambayo matokeo yake yanatarajiwa kutoa mwanga kuhusu chanzo cha vurugu na mapendekezo ya kuzuia yasijirudie. 


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalum, Profesa Palamagamba Kabudi, amesisitiza kuwa Tanzania ina rekodi thabiti ya kuheshimu haki za binadamu, demokrasia, utawala wa sheria na amani. 


Ameeleza matukio yaliyotokea yalikuwa ya kusikitisha lakini ya kipekee, hayawakilishi mwenendo wa Taifa kwa ujumla, alidokeza Katiba ya Tanzania inalinda haki za binadamu, na akaomba jumuiya ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga upya imani, kuponya majeraha ya kijamii na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.


Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, Türk ameshukuru na kupongeza uamuzi wa Rais Dkt Samia wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, akisisitiza umuhimu wa uhuru wake ili kujenga imani na kuhakikisha matokeo yenye uhalali. 


Amesisitiza njia ya mbele inapaswa kujikita katika maridhiano, uponyaji wa kitaifa na hatua za kisheria na kitaasisi zinazozingatia utawala wa sheria, huku akionesha imani na uwezo wa Tanzania kukabiliana na changamoto hizo.

No comments: