Mwandishi wetu, Monduli
maipacarusha20@gmail.com
Wananchi wa kijiji cha Selela ,Kata ya Selela,wilaya ya Monduli, mkoa Arusha, wameshukuru Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia programu ya ruzuku ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kufanikisha mradi wa maji kutoka katika chanzo cha maji cha Kabambe ambao umekuwa na manufaa makubwa.
Mradi huo, umetekelezwa na shirika la waandishi wa habari la kusaidia jamii za asili la MAIPAC ikiwa ni sehemu ya mradi wa Kuheshimu na Kulinda maarifa ya jamii za asili katika uhifadhi (Respecting and Preserving Indigenous Traditional Knowledge in Conservation) ambao pia umetekelezwa katika jamii wa Wahdzabe katika eneo la bonde la Eyasi wilaya ya Karatu.
![]() |
| Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Selela, Longidonyi Lunda akizungumza na waandishi wa habari |
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Longidonyi LundaMwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Longidonyi Lunda akiwa pamoja na viongozi wa kamati ya maji na mazingira ya kijiji hicho, alisema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa uzio kulinda chanzo cha maji cha Kabambe umeongeza maji kwani sasa hakuna tena uvamizi wa Watu, Mifugo na Wanyamapori katika eneo hilo.
Lunda alisema kwa sasa maji yanapatikana ya kutosha katika kijiji hicho, kwa ajili ya watu kunywa na kilimo ambacho kinategemea maji ya umwagiliaji na sasa heka moja inamwagiliwa kwa masaa manne tu tofauti na kabla ya kujengwa uzio wa kutunza chanzo hicho cha maji ambapo heka ilimwagiliwa kwa zaidi ya masaa sita kutokana na uchache wa maji.
Hata hivyo, alisema kwa sasa wanaomba ufadhili wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhi ili wananchi wapate maji safi ya kunywa wakati wote, kwani sasa wanapata mgao kwa kupata maji kila baada ya siku tatu.
![]() |
| Mwenyekiti wa mfereji wa kabambe Abdallah Side Mbaga akiwa katika lango la kuingia katika chanzo cha maji kabambe |
Mwenyekiti wa mfereji huo Abdallah Side Mbaga alisema mradi huo ambao umeshirikisha wananchi wa kijiji hicho, katika kufanya kazi mbali mbali umekuwa na manufaa makubwa kwani kilimo chao cha Umwagiliaji kimeimarika na sasa hakuna shamba ambalo linakosa maji ya kutosha kupitia mrefeji unaotoka chanzo cha maji ya kabambe.
"Maji ni mengi mwezi huu maeneo mengi hayana maji kutokana na ukame lakini sisi bado tuna maji ya kutosha kumwagilia mashamba na kwenda kwa wananchi"alisema
Katibu wa Mfereji huo, Yamini Paulo Mndeme alisema ujenzi wa uzio na kuimarishwa kwa mfumo wa kusambaza maji, kumeongeza uzalishaji wa mazao katika mashamba ya umwagiliaji, hasa kwa mazao ya ndizi, mbogamboga na matunda.
"tunashukuru UNDP na MAIPAC kwa mradi huu, lakini tunaomba tuendelee kuboresha mradi huu na kuwafikia wananchi wengi"alisema Mndeme
Mkandarasi wa mradi huo wa uzio wa maji na mfumo wa maji katika kijiji hicho, Ephrahimu Samweli alisema baada ya kukamilika mradi huo, kumekuwepo na ongezeko la maji kutoka katika chanzo cha maji ya Kabambe lakini kwa kuwa hawana matanki ya kuhifadhi maji hasa ya kunywa kumekuwepo na mgao wa maji.
"Mimi kama mwanakijiji wa hapa Selela, tunashukuru sana UNDP, GEF, MAIPAC na Serikali kwa kufanikiwa mradi huu na sasa tunaomba usiishie hapa maji ya kunywa yafike kwa wananchi kwa wingi bila ya mgao"alisema.
Baadhi ya wanawake ambao ni Ndemta tumbo na Mary Mollel walisema kukamilika kwa mradi huo kumeleta faraja kwao kwani sasa wanapata maji kwa urahisi.
Ndemta Tumbo alisema wanapongeza shirika la MAIPAC kwa kufanikisha mradi huo na sasa wanapata maji ya umwagiliaji na matumizi ya nyumbani kwa
Marry Mollel alisema walikuwa wakikosa maji ya uhakika ya umwagiliaji lakini sasa yanapatikana wakati wote na wanashukuru pia Serikali kwa kufanikisha kupatikana wafadhili wa miradi ya kusaidia jamii.
Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma alisema wanaamini mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na umekuja kutokana na jitihada za Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Shirika la UNDP kupitia programu ya miradi midogo na mfuko wa mazingira duniani (GEF).
"Mradi huu ambao unatekelezwa pamoja na mradi wa kukusanya maarifa ya asili katika uhifadhi kwa jamii ya Wahadzabe, unatarajiwa kuongeza vipato vya wananchi kutokana na kilimo cha umwagiliaji lakini pia kuendelea kulindwa na kuhifadhiwa chanzo cha maji ya Kabambe"alisema.
Mradi huo ni sehemu ya miradi 44 ambayo Utiaji saini ulifanyika April 4, 2024 katika Makao Makuu ya Jengo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na kuongozwa na Mwakilishi Mkaazi wa UNDP-Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara na ulizinduliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli, Isack Joseph ambaye sasa ni mbunge wa jimbo la Monduli mkoa Arusha.
MWISHO.




No comments:
Post a Comment