CCM MOROGORO YAONYA VIKALI WANAOENDELEZA SHUGHULI ZA BINADAMU NA KUHATARISHA BWAWA LA MINDU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 3 February 2026

CCM MOROGORO YAONYA VIKALI WANAOENDELEZA SHUGHULI ZA BINADAMU NA KUHATARISHA BWAWA LA MINDU

 





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


CHAMA Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Morogoro kimeonya vikali kuendelea kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo uchimbaji wa madini holela na utiririshaji wa kemikali hatarishi katika Bwawa la Mindu,


Kimesema Bwawa hilo ni chanzo kikuu cha maji kwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga, alisema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa vyanzo vya maji na baadhi ya miradi ya maji ndani ya Manispaa ya Morogoro,


Alisema uharibifu unaoendelea ni kinyume na sera za Taifa za uhifadhi wa mazingira na usalama wa maji, huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.


Masunga alisema kulinda Bwawa la Mindu ni jukumu la kila mwananchi kwa kuwa ni chanzo muhimu cha maji kwa maelfu ya wakazi, na kwamba uharibifu wake utasababisha madhara makubwa kwa afya na maendeleo ya Mkoa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Sais Kyejo, alisema mamlaka inakuja na mfumo wa kidigitali wa kubaini upotevu wa maji katika mtandao wa usambazaji, sambamba na mpango wa kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu chakavu ya maji.


Alisema hatua hizo zitasaidia kupunguza upotevu wa maji, kuongeza ufanisi wa huduma na kulinda rasilimali za maji dhidi ya uchafuzi na matumizi yasiyo endelevu.


Naye Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Sospeter Lutonja, alisema kwa sasa Mkoa una asilimia 79 ya upatikanaji wa maji, huku miradi inayoendelea ya kuimarisha upatikanaji wa maji ya uhakika ikitarajiwa kuufanya Mkoa kufikia asilimia 92 ya upatikanaji wa maji.


Alisema miradi hiyo inalenga kuongeza vyanzo vipya vya maji, kuboresha miundombinu ya kusambaza maji vijijini na kupunguza umbali wa wananchi kupata huduma hiyo muhimu.


Mwisho.

No comments: