![]() |
| WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso aagiza hati za ardhi za miundombinu ya maji kupatikana ndani ya siku 90 |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, ameziagiza mamlaka zote za maji nchini kuanza mara moja mchakato wa kupata hati miliki za ardhi kwenye maeneo yenye miundombinu yao, akisisitiza kuwa zoezi hilo likamilike ndani ya mwaka huu wa fedha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Tathmini ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/25, Waziri Aweso alisema ndani ya siku 90 kila mamlaka inapaswa kuwasilisha Wizara ya Maji na Mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Maji(EWURA) mpango kazi utakaoonesha ratiba ya upatikanaji wa hati hizo.
“Siwezi kukubali kuona miundombinu 1,352 ikiendelea kuwepo bila kinga ya kisheria,” alisema Aweso, akizitaka bodi za wakurugenzi kutenga bajeti maalum kwa ajili ya upimaji wa ardhi na usajili wa hati miliki.
Aidha, aliagiza mamlaka zilizo na miundombinu katika ardhi ya taasisi nyingine kuhakikisha zinasaini mikataba ya makubaliano (MoUs) ndani ya siku 90 ili kuepusha migogoro inayoweza kuathiri utoaji wa huduma za maji kwa wananchi.
Waziri Aweso alisema Serikali inapitia wazo la kufanya ununuzi wa pamoja wa kemikali za kutibu maji (bulk procurement) ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wakati.
Alimuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri kushirikiana na taasisi za ununuzi na mamlaka za maji kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa wazo hilo kwa kuzingatia uwazi, ushindani na thamani ya fedha.
Akizungumzia huduma ya usafi wa mazingira, Waziri Aweso alisema hali bado si ya kuridhisha, akibainisha kuwa ni asilimia 29 tu ya mamlaka zenye miundombinu ya kutibu majitaka, huku asilimia 71 zikitekeleza njia zisizo salama za utupaji wa majitaka.
Aliagiza mamlaka zote za maji kuhakikisha zinawasilisha fedha zote za tozo ya udhibiti kwa EWURA ndani ya siku 90, akionya kuwa ni marufuku kutumia fedha hizo kwa matumizi ya uendeshaji au mishahara.
“Kuanzia sasa, uwasilishaji wa tozo ya udhibiti kwa asilimia 100 utakuwa sehemu ya vigezo vya kupima utendaji wa wakurugenzi na bodi za mamlaka za maji,” alisisitiza.
Waziri Aweso alionya kuwa menejimenti zitakazoshindwa kutekeleza agizo hilo zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Waziri Aweso alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo EWURA, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk James Andilile alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya maji, bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji hatua za haraka na madhubuti ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Dk Andilile alieleza kuwa kiwango cha upotevu wa maji (Non-Revenue Water – NRW) kimeongezeka na kufikia asilimia 42.3, kutoka asilimia 36.8 mwaka uliopita, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 20.
Alifafanua kuwa upotevu huo unasababisha hasara ya mapato inayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 0.18 (bilioni 182.6), huku sababu kuu zikitajwa kuwa ni pamoja na uvujaji wa miundombinu chakavu, wizi wa maji na udhaifu wa usimamizi.
Aidha, alisema licha ya kuongezeka kwa uzalishaji wa maji, bado kiwango hicho kinakidhi asilimia 52 pekee ya mahitaji ya wananchi, hali inayosababisha uhaba wa huduma katika maeneo mengi.
Kwa upande wa upatikanaji wa maji, alibainisha kuwa wananchi bado wanapata huduma kwa wastani wa saa 14 kwa siku, jambo linaloathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, na wakati mwingine kuwalazimu kurejea kutumia vyanzo visivyo salama.
Katika eneo la kifedha, Dk Andilile alisema mamlaka nyingi za maji zinakabiliwa na changamoto ya mapato kutokidhi gharama za uendeshaji na matengenezo, hali inayohatarisha uendelevu wa huduma.
Pia alieleza kuwa asilimia 71 ya mamlaka za maji hazina miundombinu ya kutibu majitaka na tope kinyesi, jambo linalochangia uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya ya jamii.
Changamoto nyingine iliyobainishwa ni pamoja na ukosefu wa hati za umiliki wa ardhi kwa maeneo ya miundombinu ya maji, hali inayoweza kuathiri ulinzi na uendelevu wa miradi hiyo.
Kuhusu ushiriki wa sekta binafsi, alisema bado ni mdogo kutokana na mitazamo hasi, akisisitiza umuhimu wa kuunda mazingira rafiki yatakayowavutia wawekezaji kushiriki katika sekta hiyo.
Alieleza kuwa baadhi ya mamlaka zimeshindwa kuwasilisha kwa wakati tozo ya udhibiti, ambapo hadi Machi 5, 2026, kiasi cha shilingi bilioni 5.69 kilikuwa hakijawasilishwa.
Kutokana na hali hiyo, EWURA imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja ikiwa ni pamoja na kubadili mtazamo wa utendaji kazi, kuongeza ubunifu wa vyanzo vya mapato, kushirikisha sekta binafsi kupitia ubia (PPP), na kuimarisha utawala bora.
Dk Andilile pia alizitaka mamlaka za maji kuandaa mipango ya biashara, kuwasilisha maombi ya marekebisho ya bei kwa wakati, pamoja na kuongeza uwajibikaji wa bodi za wakurugenzi katika kusimamia utendaji wa menejimenti.
Alitoa wito kwa mamlaka zote za maji kuendelea kuboresha huduma kwa kuzingatia ubora, uwazi, usawa na uendelevu, na kwamba maendeleo ya sekta ya maji hayaishii kwenye uzalishaji na usambazaji pekee, bali yanategemea nidhamu ya kifedha, ulinzi wa mazingira na usalama wa miundombinu.
![]() |
Katibu mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri alisema kwa muda mrefu Rais amekuwa alisisitiza kuwa maji ni huduma ya msingi na nguzo ya ustawi wa jamii hivyo ataendelea kuhakikisha matokeo Bora yanaonekana kwa wananchi.
Akasema taarifa iliyowasilishwa na EWURA ni muhimu kwa Wizara kwa sababu inatoa tathimini nyingi za kiutendaji nanimetolewanna mdhibiti wa sekta husika kwa hiyo itasaidia kwa wakati huu ambapo Wizara inaenda kufanya tathimini.
"Taarifa hii inajibu maswaji'atano ikiwemo ya huduma zimefika kwa Kasi gani kwa wananchi, lakini Ina viashiria Saba vinavyolenga uendelevu wa miundombinu, ubora wa maji na usafi wa Mazingira, taarifa imelenga kuimarisha uwajibika,"alisema.
Pia alisema taarifa hiyo inalenga kuimarisha uwajibika,sekta binafsi ziingie kwenye uwekezaji wa maji,kama ilivyo malengo ya sera ya maji, kuboresha huduma kwa wateja na ushirikiano wa mabonde kulinda vyanzo vya maji na kuzitaka mamlaka kuitafsiri taarifa hiyo kivitendo.
Mwisho






No comments:
Post a Comment