![]() |
Mwandishi wetu, Moshi
maipacarusha20@gmail.com
Moshi.Katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Jimbo la Vunjo, Mkoani Kilimanjaro limepanda miti zaidi ya 500 ikiwa ni sehemu ya kupambana na athari za kimazingira.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Enock Koola wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika Shule ya Sekondari Mwika, kata ya Mwika Kaskazini, Kata ya Makuyuni na Kata ya Kirua Vunjo Kusini, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Aidha, Mbunge Koola, amewashukuru wadau mbalimbali walioshiriki na kuunga mkono zoezi hilo la upandaji wa miti, akisema mafanikio yake ni makubwa kwani itasaidia kukabiliana na ukame katika maeneo hayo.
Pia, Mbunge Koola ameahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira akisisitiza dhamira yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kusambaza miche ya miti na kupanua wigo wa kampeni hiyo katika maeneo mengine ya jimbo hilo.
Mbunge Koola amesema kuwa kampeni hiyo itakuwa endelevu na inahitaji ushirikiano wa wananchi wote, taasisi za elimu na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha mafanikio yake yanakuwa ya kudumu na yenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Naye, Mkuu wa Wilaya hiyo, Godfrey Mzava, amsisitiza umuhimu wa kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa ipasavyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, alielekeza kuwa kila mwanafunzi anayekabidhiwa mti awe na wajibu wa kuutunza hadi atakapomaliza masomo yake, hatua inayolenga kujenga uwajibikaji wa moja kwa moja katika utunzaji wa mazingira.
Katika kuimarisha utekelezaji wa kampeni hiyo, kampuni ya Ernst & Young imeunga mkono jitihada za Mbunge kwa kutoa miche 500 ya miti, ikiwa ni mchango wa sekta binafsi katika kusaidia maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment