Na mwandishi Wetu
maipacarusha20@gmail.com
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) imeandaa Kongamano la Wadau wa Habari, Wahariri na Waandishi wa Habari kwa mwaka 2026.
Kongamano hilo litafanyika kesho Machi 17, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ambaye atafungua rasmi kongamano hilo litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari kutoka Serikalini, Sekta Binafsi pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, wahariri na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini, Tanzania Bara na Visiwani.
Kongamano hilo linajulikana kama MISA Wadau Summit 2026 linalenga kuibua fursa za kimkakati zilizopo Mkoa wa Iringa na kujadili wajibu wa vyombo vya habari katika kuzitangaza fursa hizo ili Watanzania waweze kuzitambua na kuzichangamkia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususani kwa makundi ya Vijana .
Kwa kutambua mchango wa Serikali ya Mkoa wa Iringa chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Kheri James, MISA Tanzania imeamua kubeba kauli mbiu ya Mkoa wa Iringa isemayo: *Iringa Imara Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji.*
Ndugu waandishi wa habari, kongamano la MISA Wadau Summit 2026 lilianza Mwaka 2025 Jijini Dodoma, na mwaka huu linafanyika hapa Mkoani Iringa. Katika kongamano hilo kutakuwa na uwasilishaji wa mada mbalimbali zitakazoelezea mwelekeo wa Mkoa wa Iringa katika kuibua na kuendeleza fursa za maendeleo kutoka kwa wataalamu wa Mkoa.
Aidha, wadau wengine mbalimbali watawasilisha mada zenye kuelimisha na kufungua fursa kwa waandishi wa habari na wadau wa sekta hiyo, ikiwemo taasisi kama NSSF, PPRA, NeST na Magnina Print pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Katika siku ya pili ya kongamano Machi 18, 2026 wahariri na waandishi wa habari watapata fursa ya kufanya ziara ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambapo watajionea utajiri wa rasilimali za asili na uhifadhi uliopo katika hifadhi hiyo, na hivyo kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya utalii vya Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.
Faida za kongamano hili ni pamoja na:
1. Kukuza ushirikiano kati ya vyombo vya habari, Serikali na wadau wa maendeleo.
2. Kutoa jukwaa la kubadilishana uzoefu na maarifa kwa wahariri na waandishi wa habari.
3. Kusaidia kutangaza fursa za uwekezaji, utalii na maendeleo zilizopo katika Mkoa wa Iringa na Kuimarisha mchango wa vyombo vya habari katika kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
MISA Tanzania inapenda pia kutangaza kuwa kongamano la MISA Wadau Summit litakuwa linafanyika kila mwaka katika mikoa tofauti tofauti. Hivyo, Mkoa au taasisi zitakazopenda kuwa mwenyeji wa kongamano la mwaka 2027 zinakaribishwa kuwasiliana na uongozi wa MISA Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mapema.
Pia tunawashukuru waandishi wa habari wenzetu toka Mkoani Iringa, Serikali ya Mkoa wa Iringa kwa utayari wao wa kutupokea vyema ili mkutano huu ufanyike Mkoani hapa.
Zaidi ya washiriki 150 wanatarajiwa kushiriki kongamano letu toka Mikoa mbalimbali Bara ma Visiwani.


No comments:
Post a Comment