Na mwandishi wetu Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amewaomba wadau wa madini kujitolea na kuwasaidia waathirika wa mafuriko katika Tarafa ya Moipo.
Mwenyekiti huyo wa MAREMA Mnyawi ameyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, leo jumapili Machi 29,2026 wakati akikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mwalimu Fakii Raphael Lulandana vyakula na vifaa vya thamani ya shilingi milioni 22 vilivyotolewa na kampuni ya Permanent Mining LTD kwa ajili ya waathirika wa mafuriko katika Tarafa ya Moipo.
Ameeleza kuwa japokuwa wachimbaji madini wamekuwa wakijitoa mara kwa mara kupitia hisani kwa jamii (CSR) wasiliache hilo likapita bila kuchangia chochote.
Amesema wachimbaji mbalimbali ikiwemo Franone Mining, God Mwanga, Chusa Mining, California Camp, Bilionea Saniniu Laizer, Sunda Mining wamekuwa wakisaidia jamii wasaidie pia waathirika hao waliokumbwa na mafuriko.
"Kupitia hadhara hii nampongeza Mkurugenzi wetu God Charity ambaye baada ya Mbunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Millya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufikisha ombi la msaada kwa waathirika wa mafuriko alikubali ombi hilo mara moja," amesema Elisha Mnyawi.
Amesema wadau wa madini wamekuwa na moyo wa kujitolea hivyo anaamini watafanikisha kuwapatia misaada zaidi wakazi hao wa tarafa ya Moipo waliokumbwa na mafuriko.
"Mheshimiwa DC wachimbaji madini wana moyo wa kujitolea mno tumeona Franone Mining wanajitolea kujenga zahanati migodini, Chusa Mining anajenga wodi za wanawake kituo cha afya Mirerani utaona na hili janga la waathirika wa mafuriko wanajitokeza kusaidia," amesema Mwenyekiti huyo wa MAREMA.
Ametaja msaada uliotolewa na Performance mineral LTD ni mahindi magunia 100, mafuta ya kupikia madumu 318, mashuka 100, mchele kilo 500, sabuni 400, mafuta ya kujipaka katoni 20 na vyandarua 100.
Ametaja vitu vingine ni madaftari 100, kalamu 200, penseli 200, kompasi 100, malapa katoni sita na chumvi katoni sita.
Hata hivyo, DC Simanjiro mwalimu Fakii Raphael Lulandana amesema watu 1,163 wameathirika kwa mafuriko katika Tarafa ya Moipo.
Mwalimu Lulandana amesema pia ekari 5,429 za mashamba ya mazao ya maharage na mahindi yameathirika kwa kusombwa na maji katika eneo hilo.
Frank Oleleshwa ambaye ni katibu wa mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema kiongozi huyo yupo nje ya nchi Guinea ya Ikweta na anatoa pole nyingi kwa wapiga kura wake.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Hans Nkya amemshukuru God Mwanga kupitia kampuni ya Permanent Mining LTD kwa kusaidia waathirika wa mafuriko katika Tarafa ya Moipo.
MWISHO

No comments:
Post a Comment