NMB yawazawadia kompyuta mpakato watumiaji bora wa Flexi-Malipo - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 9 March 2026

NMB yawazawadia kompyuta mpakato watumiaji bora wa Flexi-Malipo

 

 




Na mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com 


Moshi. Benki ya NMB imekabidhi zawadi mbalimbali kwa watumiaji  bora wa  mfumo wa Flexi-malipo kwa shule mbalimbali nchini unaolenga kupunguza foleni na kurahisisha ulipaji wa ada za shule kidigitali.


Akikabidhi zawadi hizo ikiwemo kompyuta mpakato kwa wamiliki hao kutoka sehemu mbalimbali nchini, Meneja wa benki hiyo Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus, amesema mfumo huo unarahisisha ulipaji wa ada na kupunguza foleni benki kwa wazazi wa wanafunzi, hivyo kuongeza urahisi na ufanisi wa huduma za kifedha.


Amesema, kwa miaka ya nyuma, wazazi  walilazimika kupanga foleni benki ili kulipa ada hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa muda wa kazi na wakati mwingine kupoteza fedha au risiti huku walimu wakitumia muda mwingi kufuatilia malipo.


Amesema kupitia kampeni hiyo wamepata washindi bora 20 kutoka mikoa mbalimbali kwa kutumia kwa wingi miamala ya malipo ya ada kupitia mfumo huo wa Flexi-malipo. 



Mmoja wa washindi hao,  kutoka shule ya Sekondari ya wavulana ya  St Joseph, Calvin Makyao, amesema mfumo huo umewasaidia kwa kiasi kikubwa kwani mzazi anayelipa ada mfumo huo unamtambua kwa majina na kiasi ambacho kimelipwa, hivyo kupunguza usumbufu wa kuuliza wanafunzi risiti.


"Kampeni hii imetusaidia kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.Kipindi cha nyuma wazazi walikuwa wanahangaika na kuteseka lakini sasahivi imeturahisishia kwani malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa ufanisi na kumbukumbu zimekuwa zikiwekwa vizuri,"amesema 


Akizungumza mwalimu kutoka shule ya Archangels, Sista Marygoreth Tarimo, amesema awali walikuwa wakipata changamoto ya kujua ni mwanafunzi gani amelipa ada lakini kwa kutumia mfumo huo umewarahishia kupata taarifa sahihi za malipo ya mwanafunzi.


"Kwa kutumia mfumo huu wa control namba imetusaidia sana pale shuleni kwasababu mwanzoni tulikuwa tukiteseka sana hasa katika kutambua mfumo ambao bado hawajalipa, mara nyingi ilikuwa ni changamoto kwasababu unaweza kumdai mzazi kumbe ameshalipa na mwingine hajalipa hivyo ilikuwa ikituchanganya,"amesema 


Mwisho.

No comments: