Na Mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
OFISI ya Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma imezindua mfumo wa kusikiliza kero za wananchi kidigitali kupitia namba maalumu WhatsApp ijulikanayo kama Chemba konektedi.
Kupitia namba hiyo maalum ya 0771400500 itakayotumika kwa mfumo wa WhatsApp wananchi wataweza kuwasilisha kero na changamoto zao moja kwa moja bila kutumia muda, nauli kwa kusafiri kwenda katika ofisi ya mkuu wa Wilaya, idara na taasisi za Umma katika Halmashauri ya Chemba.
Akizungumzia kuhusiana na hatua hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chemba Halima Okash amesema kupitia Chemba Connect WhatsApp chatbot mwananchi ana uwezo wa kutuma malalamiko yake, kero na changamoto mbalimbali na kujibiwa ndani ya saa 24.
Pia Okash amesema kupitia Chemba Konektedi ya whatsapp wananchi na wadau wa ndani na nje ya wilaya hiyo wana uwezo wa kupata taarifa ya fursa mbalimbali zinazopatikana katika Wilaya hiyo zikiwemo za kilimo,utalii, uwekezaji na pia kujua idara zinazopatikana na huduma zinazotolewa katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya namba hiyo maalumu ambayo ofisi yake imeipata yeyote atakayepiga ataunganishwa moja kwa moja na ofisi yake pia mwananchi anaweza kuingia whatsapp moja kwa moja na kuandika ujumbe wake kuhusiana na kero inayomkabili.
"Mpango huu Mhe. Rais alikua anatamani sana ufanyike kuwarahisishia wananchi namna ya kuwasilisha kero zao kwa wakati ili ziweze kushughulikiwa na hii itarahisisha pia kujua kazi zinazofanywa na Wilaya hiyo moja kwa moja kupitia njia ya kidigitali," amesema
Okash, amewasisitiza wananchi kutumia mfumo huo rahisi na haraka katika utatuzi wa kero, changamoto na fursa mbalimbali zinazohusu Wilaya ya Chemba.
Wakizungumzia kuhusiana na mpango huo wa chemba konektedi baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo akiwemo Jamali Juma kutoka Kijiji cha Magandi amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuanzisha utaratibu mpya wa kuwasilisha kero zao kupitia namba maalumu.
Juma amesema utaratibu huo utawarahisishia kufikisha taarifa kwa mkuu wa wilaya kuhusiana na mambo mbalimbali yanayotokea kwenye maeneo yao ikiwemo kero zilizopo ndani ya jamii ziweze kufika kwa wakati na kushughulikiwa bila kusubiri mikutano na ziara za viongozi
Mmoja wa Vijana kutoka kijiji cha Magandi Joshua Vicent naye amemshukuru Okash kwa kuanzisha mfumo wa kidigitali ambao unakwenda kuwarahisishia kufikisha kero zao jambo ambao litaokoa muda na gharama waliyokuwa wakiitumia awali kuifikia ofisi ya Mkuu wa Wilaya na idara mbalimbali katika ofisi ya Mkurugenzi. .
Kadhalika Sakina Juma amesema wapo wananchi ambao kuzungumza kwenye mikutano kwao ni shida lakini kupitia mfumo huo watawasilisha kero zao sehemu husika kwa wakati.
Wananchi hao wamesema kupitia mfumo huo popote mwananchi alipo atawasilisha kero zake bila kusubiri mikutano ama ziara ya mkuu wa wilaya na viongozi wengine kwenye kijiji chao na hiyo itawapa nafasi ya kufanya shughuli zao za Maendeleo kwa kuokoa muda na gharama.
Mpango huo wa Chemba Connect WhatsApp chatbot kupitia namba maalumu unapatikana kwa saa 24 siku 7 zote za wiki.
Mwisho


No comments:
Post a Comment