RC MAKALLA AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI MKOA WA ARUSHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 31 March 2026

RC MAKALLA AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI MKOA WA ARUSHA

 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla akisalimiana na viongozi wa dini 





- *_Atoa Tamko la baadhi ya Viongozi wa mila kuwajeruhi, kuwakamata Viongozi wa dini na kufungia makanisa kuhusiana na tohara_* 


- ⁠ *_Akemea vitendo hivyo na kutaka jeshi la polisi kuchukua hatua za haraka kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote wanaofanya vitendo hivyo_* 


. *_Aagiza Wakuu wa Wilaya kupitia kamati za ulinzi kusimamia maelekezo hayo na kufanya vikao vya viongozi wa dini na viongozi kimila_* 


. *_Awaomba viongozi wa dini kuombea Taifa amani na kuwataka kujiepusha na migogoro ndani ya taasisi za dini_*


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumanne Machi 31, 2026 katika Kikao chake na Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali Mkoani Arusha ametoa tamko na kukemea vitendo vya baadhi ya Viongozi wa Kimila kuwajeruhi, kuwakamata Viongozi wa dini na kufunga Makanisa kutokana na mila na tohara kwa baadhi ya Makabila.

Viongozi wa dini wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla

Mhe. Makalla amekemea vitendo hivyo akisisitiza Amani, umoja na mshikamano kwa wananchi na kuliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka za kuwakamata na kuwafikisha kwenye Vyombo vya sheria wale wote wanaohusika na vitendo hivyo, akivitaja kama vya kihalifu, visivyokubalika na vyenye kudhohofisha uhuru wa kuabudu kwa wananchi.


"Hili la mgogoro ambalo limekuwa likisababisha mivutano kuhusiana na mafundisho ya Kanisani na ya mila na tohara na baadae kuwakwaza Viongozi wa dini na kuhatarisha amani kwa kuwakamata, kuwafanyia vitendo viovu viongozi wa dini, kuingilia ibada zao na kuchukua hatua za kufunga Makanisa hayo ni kinyume na sheria na atakayefanya hivyo ni muhalifu kama wahalifu wengine na halikubaliki na kwa dhamana niliyonayo ninao wajibu wa kuhakikisha Mkoa unakuwa salama." Amekaririwa Mhe. Makalla.


Aidha Mhe. Makalla amewataka Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati za ulinzi na usalama kusimamia maelekezo hayo na kufanya vikao na Viongozi wa dini na wa kimila ili kuwajengea uelewa wa pamoja Viongozi hao ili kukomesha tabia hiyo, akisisitiza umoja na mshikamano na kuahidi kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa maelekezo yake, akiwaomba pia Viongozi hao wa dini kuendelea kuliombea Taifa amani na kujiepusha na migororo ya ndani ya Taasisi za dini, akisema uimara na umoja miongoni mwao ni afya kwa serikali na jamii ya Tanzania.

No comments: