Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha20@gmail.com
WANAWAKE wa Mkoa wa Manyara, wamempongeza kwa kumpatia tuzo Mkuu wa Mkoa huo Queen Cuthbert Sendiga kwa namna anavyoongoza kwa utawala bora na uliotukuka katika Mkoa huo.
RC Sendiga amekabidhiwa tuzo hiyo na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala Lulandala kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kimkoa yamefanyika kwenye kijiji cha Orkirung'rung' Kata ya Edonyongijape.
DC Lulandala amesema amekabidhi tuzo hiyo kwa RC Sendiga kwa kutambua uongozi thabiti na utawala bora kwa wananchi wa mkoa wa Manyara.
"Wanawake wa mkoa wa Manyara wametambua juhudi zako katika kujitoa kwako kuwatumikia na kuhakikisha jamii unayoingoza inapata maendeleo na kuishi kwa amani na utulivu," amesema DC Lulandala.
RC Sendiga akizungumza kwenye maadhimisho hayo amewashukuru wanawake hao kwa kutambua mchango wake na kumtunuku tuzo hiyo waliyompatia.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo amewaasa wanawake hao kutumia mbinu 223 na siyo mbinu moja za kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika familia zao na jamii kwa ujumla.
"Mwanamke anapaswa kuleta mabadiliko ya dunia kila mahali alipo na usisubiri uwe kiongozi na dunia itakuwa njema zaidi kupitia mwanamke," amesema RC Sendiga.
Amesema wanawake wanapaswa kung'ara katika nyanza zote ikiwemo kiuchumi, kiuongozi, kielimu, kimalezi ya watoto, kuondokana na watoto wenye utapiamlo na wenye udumavu.
"Wakina baba hawali chakula na kushiba nyumbani, mnawaacha wazunguke na vichupa vya pombe mitaani, bado wanawake wanapaswa kuwatunza wanaume," amesema RC Sendiga.
Msoma risala Belinda Sumari amesema pamoja na jitihada za serikali kuwajengea uwezo wa kiuchumi kwa wanawake wamepatiwa elimu ya malezi na makuzi, haki za wanawake na kupinga ukatili.
Hata hivyo, amesema bado wanawake na wasichana wana changamoto za ukosefu wa mitaji ya kuanzisha ujasiriamali katika eneo hilo.
Amesema wanawake wa mkoa wa Manyara wanaendelea kupambana na ndoto zao na ndogo za watoto wao zisizimwe na changamoto kwani kila changamoto ni daraja la kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Baadhi ya wadau wa maendeleo wa mkoa huo Taiko Kulunju na Mula Sanare Lesiangiki wamepatiwa vyeti vya kufanikisha maadhimisho hayo.
MWISHO

No comments:
Post a Comment