![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Media Brains, Jesse Kwayu akiwasilisha mada katika mafunzo hayo |
![]() |
ANDREA NGOBOLE, maipac
maipacarusha20@gmail.com
Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuhakiki taarifa zao kabla ya kuandika na kusambaza Habari mtandaoni ili kuepuka kusambaza habari potofu kwa jamii ama zenye chumvi.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Media Brains, Jesse Kwayu, amesema hayo katika mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Arusha ambapo amesisitiza kuwa wanapaswa kuwa makini na vyanzo vya habari kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Media Brains kwa udhamini wa Taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS) ya Ujerumani kwa waandishi wa habari 20 wa mkoa wa Arusha, yalilenga kuwajengea uwezo waandishi kuandika na kuripoti habari za mtandaoni kwa usahihi bila kuathiriwa na mazingira ya usambazaji wa taarifa feki mtandaoni.
Kwayu akiwasilisha mada ya misingi thabiti ya uandishi wa habari za kidijitali alisema kuwa kwa sasa tasnia ya habari imebadilika kwa kiasi kikubwa na kuhamia zaidi kwenye majukwaa ya mtandaoni, hali inayohitaji waandishi wa habari kujifunza mbinu mpya za uandishi pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili unde (AI) katika ukusanyaji na uchakataji wa taarifa.
“Waandishi wa Habari za mtandaoni ni lazima mzingatie fact checking kabla ya kuandika na kuripoti tukio la Habari ili mjikinge na madhara ya kusambaza Habari potofu na kujiletea matatizo ya kisheria, pia mkumbuke Habari za mtandaoni zinapaswa kuwa fupi, sahihi na zinazingatia mambo muhimu tu kabla ya kupost mtandaoni” Alisisitiza katika mafunzo hayo
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Media Brains, Absalom Kibanda akiwasilisha mada uandishi wa habari mitandao ya kijamii na ushiriki wa jamii unaotoa fursa kwa wasomaji kukosoa na kutoa majibu ya haraka pale habari inapokuwa na maslahi mapana kwao, amesema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kutambua taarifa za uongo na uzushi ambazo zimekuwa zikisambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii hivyo ni vema kujiuliza mara mbili je taarifa unayotaka kuipost katika mtandao wa kijamii ni sahihi kabla ya kuiweka mtandaoni.
Baadhi ya waaandishi wanufaika wa mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa taarifa zisizo sahihi katika mitandao ya kijamii, hali inayotokana na kukua kwa teknolojia na urahisi wa kusambaza habari kupitia mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu, ameshukuru media brains kwa kutoa mafunzo hayo kwa wanahabari hao ambapo waandishi waliopata mafunzo hayo wanatarajiwa kuwa mfano kwa wengine kwa kuhakikisha wanazingatia maadili ya taaluma na kuepuka kusambaza habari zisizo na uthibitisho katika majukwaa ya mtandaoni.
##Mwisho##







No comments:
Post a Comment