📌Bil 6 yawezesha kusambaza miundombinu ya Gesi asilia kwenye kaya 1,000
Na Lilian Kasenene,Pwani
maipacarusha20@gmail.com
WAKALA wa Nishati Vijijini(REA) umetoa wito kwa wananchi wa Mikoa ya Pwani na Lindi unakopita mradi wa usambazaji wa gesi asilia kuchangamkia fursa ya mradi huo ambapo mpaka Sasa kaya 1,000 zimenufaika.
KAIMU meneja usaidizi wa kiufundi kwa uendelezaji miradi kutoka REA, Mhandisi Emanuel Yesaya alieleza hayo wakati wa ziara ya kikazi ya wahariri walipotembelea mradi wa usambazaji wa Gesi asilia kwenye nyumba za makazi eneo la Kisemvule mkoani Pwani.
Mradi huo wa kimkakati unaofadhiliwa na REA, unasimamiwa na kutekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Mhandisi Yesaya alisema Rea wamekuwa wakifadhili miradi ya aina mbalimbali hivyo wananchi hao ni vyema wakachangamkia fursa hiyo ili kuweza kujiunga na kupata faida ya miradi inayofika kwenye maeneo yao.
REA imefadhili mradi wa usambazaji wa Gesi asilia katika eneo la mnazi mmoja Kata ya mingoyo mkoa ya Lindi na kisemvule Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani, ambapo mradi huo unanufaisha jumla kaya 1,000 na taasisi Moja ambazo zimefikishiwa miundombinu ya Gesi asilia.
Alisema mradi huo umejengwa katika maeneo ambayo Bomba kubwa la Gesi asilia kutoka Mkoa wa Mtwara kwenda Dar es salaam limepita ambapo ilikuwa mradi wa kimkakati kwa ajili ya kuwezesha wananchi kutumia Nishati safi za kupikia katika nyumba yao.
Aidha, mradi huo umefadhiliwa na REA kwa kiasi cha sh bilioni 6.8 ambazo zilipelekwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC ambao ndio wasimamizi na wanatekeleza wa mradi huo na kwamba tayari mradi imekamilika tangu Januari 2026.
"Kukamilika kwake ni kwamba tayari zile kaya zote 470 na taasisi Moja eneo la Lindi na kaya 530 za eneo la Kisemvule Pwani zimeweza kupatiwa mita za Gesi asilia na wananchi wanatumia na kunufaika na mradi huu,"alisema Mhandisi Yesaya.
Alisema mradi huo ulifanyika kwa nia kusaidia wananchi kutumia Nishati safi na kusaidia kuepukana na magonjwa yanayoweza kutokea kwa kutumia Nishati zisizosafi za kupikia kama kupumua, pamoja na kuwezesha kulinda Mazingira na kupunguza ukataji wa Misitu na matumizi ya Kuni na mkaa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mhandisi Yesaya alisema cha muhimu kwa mradi huo ni jinsi suala la matumizi kuwa gharama nafuu kwamba kila kaya imefungia mita ambayo inaweza kununua Gesi kwa njia ya simu kwa kutumia namba ya kumbukumbu ambayo anaweza kutumia kununua kiwango cha Gesi ambacho kinaanzia sh 1,000.
"Mradi huu ni mzuri ambao Serikali kupitia Rea wameweza kuufadhili na pia tunaangalia kuweza kuongeza wigo kwa awamu nyingine kuweza hufadhili zaidi miradi ya namna hii ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, tunalipongeza shirika la TPDC kwa kufanya mradi kwa viwango vinavyotakiwa kwa muda uliokuwa umewekwa kwa mujibu wa mkataba wa mradi,"alisema.
Mhandisi kutoka TPDC Antony Kayomba alisema wao kama watekelezaji wa mradi huo ulioanza machi 2025 umekamilika na jumla ya umbali walioweza kukamilisha ni kilometa 56.56 kwa Mikoa ya Lindi kilometa 31.33 na Kisemvule Pwani kilometa 25.23 .
Alisema Wateja wamekuwa wakilipankwanza ndo wanafanya matumizi na kwamba usalama kwa wateja ni Salama zaidi.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kitangwi Kijiji cha Kisemvule Kata ya Vikindu Hussein Shemndolwa aliishukuru Serikali kwa kuwaletea.mradi huo kwani wananchi waliopata huduma hiyo wamenufaika.
Aliomba Serikali kuongeza zaidi huduma hiyo ya mradi wa usambazaji wa Gesi kwani wananchi wengi bado wanahitaji ambapo alieleza kuwa katika eneo hilo la Kisemvule kuna kaya zaidi ya 12,000 hivyo mahitaji bado ni makubwa.
"Serikali ya kijiji kwa sasa Iko kwenye ujenzi wa jiko la shule ya msingi Kisemvule kwa ajili ya kufungwa mitambo na majiko ili watoto waweze kupata uji na chakula kwa wanafunzi wetu,"alisema Shemndolwa.
Mmoja wa wanufaika na mradi huo Mariam Sekena alisema matumizi ya Gesi asilia yanasaidia sana wananchi na ni nafuu ya kuanzia sh 1,000 tofauti na awali walivyokuwa wakitumia gharama kubwa ya sh 25,000.
Alisema kaya yake yenye watu watatu awali walikuwa wakilazimika kutumia kuni na mkaa kwa ajili ya upishi pindi nishati inapoisha na kwamba tangu alianza kutumia nishati ni mwezi wa pili Sasa.
Afisa mtendaji mkuu wa Jukwaa la wahariri Tanzania(TEF) William Shao, alipongeza REA kwa ufadhili wa mradi huo na kuwaomba kuendelea kufadhili zaidi kwa miradi mingine itakayofuata.
"Mambo kama yataendelea kuwa hivi kama tulivyoelezwa, Ina maana baadae Hali itakuwa njema sana hasa kwa gharama za watu wengi kuepuka hizi gharama za Nishati chafu ya kupikia na kuendana na Nishati safi,"alisema Shao.
Mwisho.l



No comments:
Post a Comment