Wanaume TANAPA Waunga Mkono Wanawake Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 8 March 2026

Wanaume TANAPA Waunga Mkono Wanawake Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani

 






Na Pamela Mollel,Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


 Wanaume wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wamepongezwa kwa kuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika bonanza la michezo na afya lililofanyika jana tarehe 7 machi,kama sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za uhifadhi.



Akizungumza katika bonanza hilo lililojulikana kama TANAPA Sport Health Day, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Kamanda wa Kanda ya Kaskazini wa TANAPA, Steria Ndaga, aliwashukuru wanaume wa shirika hilo kwa kujitokeza kwa wingi na kuwa mstari wa mbele katika kushiriki na kusaidia kufanikisha shughuli hiyo


Ndaga alisema ushiriki huo unaonesha mshikamano uliopo ndani ya shirika hilo, huku akiwapongeza pia wanawake wa TANAPA kwa kujitokeza tangu asubuhi na kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali licha ya majukumu makubwa waliyonayo katika kazi za uhifadhi.


Alisisitiza kuwa wanawake ni sehemu muhimu ya shughuli za uhifadhi, akibainisha kuwa wanafanya kazi bega kwa bega na wanaume katika kulinda rasilimali za taifa ndani ya hifadhi mbalimbali.


Bonanza hilo lilifanyika katika viwanja vya AIM Mall, jirani na Ofisi za Makao Makuu ya TANAPA, na lilihusisha pia watumishi kutoka hifadhi za karibu waliokuja kushiriki katika michezo mbalimbali.


Miongoni mwa michezo iliyofanyika ni mbio za kilometa tano na kumi, mpira wa miguu, kuvuta kamba, kufukuza kuku, kukimbia na mayai pamoja na mbio za magunia, huku washindi wakijizolea zawadi mbalimbali.


Mbali na michezo, washiriki walipata huduma za afya kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ikiwemo upimaji wa uzito, sukari, presha na VVU, pamoja na elimu ya kukabiliana na majanga ya moto iliyotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutoka Arusha.

No comments: