Na Lilian Kasenene, Njombe
maipacarusha20@gmail.com
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa ruzuku ya Sh bilioni 1.63 kuwezesha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa maji wenye uwezo wa kilowati 360 wa Ijangala uliopo Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Umeme unaozalishwa na mradi huo tayari umeunganishwa katika Gridi ya Taifa, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji na uimara wa nishati ya umeme katika maeneo ya vijijini.
Kaimu Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emanuel Yesaya, alieleza hayo mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walipotembelea mradi huo uliopo Kijiji cha Masisiwe, Kata ya Ukwama katika Wilaya ya Makete.
Alisema ruzuku iliyotolewa na REA imewezesha ujenzi wa miundombinu muhimu ya mradi huo wa kuzalisha umeme wa maji unaojulikana kama Ijangala Mini Hydropower Plant wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 360 na kuingiza umeme huo kwenye Gridi ya Taifa.
“Yes, huu ni miongoni mwa miradi ya uzalishaji umeme iliyopata msaada wa Serikali kupitia REA kuanzia hatua ya upembuzi yakinifu hadi maandalizi ya utekelezaji. Serikali pia ilitoa ruzuku kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari za mazingira pamoja na maandalizi ya design plan ya mradi,”alisema Mhandisi Yesaya.
Alifafanua kuwa juhudi za Serikali kupitia REA zimekuwa zikilenga kusaidia taasisi za serikali na sekta binafsi kuanzisha miradi ya kuzalisha umeme, hatua inayochangia kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa pamoja na kuimarisha ubora na uthabiti wa nishati nchini.
Mradi huo unatekelezwa na Dayosisi ya Kusini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kupitia Kituo cha Udiakonia cha Tandala, kwa ushirikiano na Serikali kupitia REA katika kukuza uwekezaji kwenye nishati jadidifu vijijini.
Mhandisi Yesaya alisema mbali na ruzuku ya Sh bilioni 1.63, mradi huo pia ulipata mkopo nafuu wa Sh milioni 922 kupitia programu ya Tanzania Rural Electrification Expansion Program (TREEP) unaosimamiwa na REA, uliosaidia kugharamia shughuli za ujenzi na mahitaji mengine ya mradi.
Alisema Serikali pia imegharamia vifaa na miundombinu muhimu ikiwemo transfoma chochezi yenye uwezo wa KVA 500 pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 0.6 inayounganisha kituo hicho na Gridi ya Taifa inayosimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania.
Kwa mujibu wa Yesaya, mradi wa Ijangala ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, huku Mkoa wa Njombe ukiwa na zaidi ya miradi mitano inayozalisha umeme na kuuza kwenye Gridi ya Taifa au kusambaza moja kwa moja kwa wananchi kwa leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania TEF, Deodatus Balile, aliipongeza REA kwa uwekezaji huo na kushauri Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji katika miradi ya nishati vijijini.
“Sisi TEF tumejionea kwa macho kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kupitia REA kwenye mradi huu. Miradi kama hii ina mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa umeme kwa wananchi na kukuza maendeleo ya Taifa,” alisema Balile.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Umeme wa Ijangala, Daudi Sanga, alisema mradi huo umefadhiliwa kwa kiasi kikubwa na REA pamoja na wadau wa maendeleo, na kwa sasa unazalisha kilowati 360 zinazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Alisema mradi huo ulianza mwaka 2025 na hadi sasa miundombinu muhimu ikiwemo bwawa, mabomba ya kusafirisha maji, power house pamoja na substation imekamilika, huku uzalishaji na uuzaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa ukiwa umeanza rasmi.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment