THRDC yatoa tamko" zito" madhimisho siku ya wanawake duniani. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 8 March 2026

THRDC yatoa tamko" zito" madhimisho siku ya wanawake duniani.




Mwandishi wetu.


maipacarusha20@gmail.com

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)umeungana na jumuiya ya kimataifa katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, huku ikikemea matukio ya kuzuiwa baadhi ya wanawake kushiriki katika maadhimisho hayo.


Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu mratibu wa THRDC Kwa niaba ya wanachama, Wakili Halima Sonda amesema maadhisho haya ambayo yanaadhimishwa kila mwaka yanatambuliwa rasmi ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1975 wakati wa Mwaka wa Kimataifa wa Wanawake (International Women’s Year).


Kaimu mratibu wa THRDC, Wakili Halima Sonda

Wakili Sonda amesema ya kutambua maadhimjsho hayo ilikuwa sehemu ya juhudi za kimataifa za kuimarisha usawa wa kijinsia, kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii, na kuhimiza nchi wanachama kuchukua hatua za kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake.


Amesema baadaye mwaka 1977, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio Na. 32/142 lililozihimiza nchi wanachama kutambua siku maalum ya haki za wanawake na amani ya kimataifa (United Nations Day for Women’s Rights & International Peace). Tangu wakati huo, nchi nyingi duniani zimeendelea kuitambua na kuadhimisha tarehe 8 Machi kama Siku ya Wanawake Duniani, ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kitamaduni pamoja na kutathmini hali ya haki za wanawake duniani.

Aidha, umuhimu wa siku hii unaimarishwa pia na mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kulinda na kukuza haki za wanawake. Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake
(Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women – CEDAW) wa mwaka 1979, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Itifaki yake kuhusu Haki za Wanawake barani Afrika (Maputo Protocol). Mikataba hii inaweka wajibu kwa nchi wanachama kuhakikisha usawa wa kijinsia na kulinda haki za wanawake katika nyanja zote za maisha ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa mujibu wa misingi ya haki za binadamu inayotambuliwa kimataifa, siku za kimataifa
za haki za binadamu hutumika kama fursa ya kutoa elimu ya haki, kuongeza uelewa, kufanya tathmini ya hali ya haki za binadamu, na kuhamasisha jamii pamoja na serikali kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi wa haki hizo.

Siku ya Wanawake Duniani ni miongoni mwa siku muhimu za haki za binadamu zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na pia husherekewa katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania.

Katika muktadha huo, Watanzania wote, makundi mbalimbali katika jamii, na hasa watetezi wa haki za binadamu, wana haki ya kuadhimisha siku za haki za binadamu kama zinavyotambuliwa kimataifa na kitaifa.

Kwa miaka mingi, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umekuwa ukitoa elimu ya haki za binadamu kwa umma na watetezi wa haki na kuhamasisha umuhimu wa kuadhimisha siku mbalimbali za haki za binadamu kama njia ya kukuza uelewa wa haki hizo na kujenga jamii inayoheshimu utu wa binadamu.


Kwa miaka mingi pia, wanawake kupitia Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) wamekuwa wakiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya mikutano na makongamano katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa mfano, tarehe 8 Machi 2023 mkoani Kilimanjaro, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishiriki kama mgeni rasmi katika kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lililoandaliwa na BAWACHA, jambo linaloonyesha kuwa maadhimisho haya ni sehemu ya utamaduni wa kitaifa unaotambua umuhimu wa haki za wanawake.

Wakili Sonda anasema siku ya Wanawake Duniani si tu siku ya kusherekea mafanikio ya wanawake, bali pia ni siku ya kufanya tathmini ya hali ya wanawake katika jamii, kujadili changamoto zinazowakabili, kutathmini ukiukwaji wa haki zao, na kuibua mikakati ya kuondoa ukiukwaji wa haki zao.



Anasema Wanawake wana haki ya kukutana, kujadili na kusherekea siku hii muhimu kama sehemu ya utekelezaji wa haki zao za msingi.


Hata hivyo anafafanua kuwa, Mtandao umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za matukio yaliyotokea
kati ya tarehe 6, 7 na 8 Machi 2026, ambapo Jeshi la Polisi limezuia misafara ya wanawake
wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
waliokuwa wakielekea Musoma kwa lengo la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Wanawake hao walizuiwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwemo Mlandizi, Dumila, Gairo, Geita, Dodoma, Bunda na maeneo mengine.


Anasema tukio hili linafanana na matukio yaliyowahi kutokea hapo awali ambapo shughuli
za kiraia zinazohusiana na maadhimisho ya siku za haki za binadamu au mikusanyiko ya kijamii zimezuiwa.




 Mfano wa tukio hilo ni lililotokea mwezi Agosti mwaka 2024 jijini Mbeya ambapo Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) lilipanga kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Kabla ya maadhimisho hayo kufanyika, Jeshi la Polisi lilizuia mkusanyiko huo na kuwakamata viongozi pamoja na mamia ya vijana waliokuwa wakielekea Mbeya kushiriki katika shughuli hiyo, huku zaidi ya watu 500 wakiripotiwa kukamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unasikitishwa na unalaani vitendo hivyo, kwani vinakinzana na misingi ya haki za binadamu pamoja na haki zinazolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakili Sonda anasema kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mtu ana haki ya uhuru wa maoni na kujieleza pamoja na haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa. Aidha, Ibara ya 20 ya Katiba inalinda haki ya watu kukusanyika na kuungana kwa madhumuni halali bila kuingiliwa bila sababu za msingi zinazotambuliwa kisheria. Kuzuia wanawake kusafiri au kukutana kwa lengo la kuadhimisha siku ya haki za wanawake kunakiuka misingi hii ya kikatiba. Vilevile, Tanzania ni mwanachama wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki zabinadamu ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) na
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ambayo inalinda haki za kukusanyika kwa amani, kujieleza na kushiriki katika shughuli za kijamii na kisiasa bila ubaguzi.


Zaidi ya hayo, moja ya misingi muhimu ya haki za binadamu ni haki ya kila mtu kufurahia haki zake za msingi (the right to enjoy fundamental human rights). Hivyo, kitendo chochote cha kuzuia wanawake kuadhimisha siku yao muhimu kinakiuka misingi hiyo pamoja na utamaduni wa kimataifa wa kuheshimu na kuadhimisha haki za wanawake.


Mtandao unaamini kuwa Siku ya Wanawake Duniani inapaswa kuadhimishwa na wanawake wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, vyama wanavyotoka au makundi yaokatika jamii. Haki za wanawake ni haki za binadamu, na ulinzi wake haupaswi kuathiriwana tofauti za kisiasa.

Kutokana na hali hiyo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unatoa wito ufuatao:


1.  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa wanawake wote wanaruhusiwa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani na siku nyingine za haki za binadamu bila vikwazo.

2. Jeshi la Polisi kuzingatia wajibu wake wa kikatiba wa kulinda haki na usalama wa
raia badala ya kuzuia shughuli halali za kijamii zinazolenga kuadhimisha haki za binadamu.

3. Taasisi zote za umma kuheshimu na kuwezesha Watanzania kushiriki katika maadhimisho ya siku za haki za binadamu zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na zile zinazotambuliwa kitaifa.

4. Wanawake na makundi yote katika jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika
majadiliano na harakati za kuimarisha haki za wanawake, usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamiii

5. Wito kwa Watetezi, Makundi ya Kjamii kuendelea kuazimisha siku mbalimbali za haki za Binadamu huku mkizingatia Malengo ya kila siku husika na kuzingatia misingi yote ya ya utulivu na amani.


Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unaendelea kusisitiza kuwa haki za binadamu ni za wote na zinapaswa kulindwa bila ubaguzi wowote.

 Kuadhimisha siku za haki za binadamu ni sehemu muhimu ya kujenga jamii inayoheshimu utu wa binadamu, usawa na haki.


Mwisho

No comments: