VIONGOZI WA UMMA WATAKIWA KUWA KIELELZO CHA UAMINIFU 📌Mameya,Wenyeviti wa Halmashauri nchini wakutanishwa kwenye mafunzo ya maadili - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 25 March 2026

VIONGOZI WA UMMA WATAKIWA KUWA KIELELZO CHA UAMINIFU 📌Mameya,Wenyeviti wa Halmashauri nchini wakutanishwa kwenye mafunzo ya maadili

 







Na Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com 


VIONGOZI wa umma wametakiwa kuwa kielelezo cha uaminifu, uwazi, usawa na uzingatiaji sheria katika maamuzi yao ya kila siku.


Kamishna wa maadili ofisi ya rais sekretarieti ya maadili ya viongozi, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi  amesema maadili yanasaidia kuzuia migongano ya maslahi, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na upendeleo.


"Maadili hujenga utamaduni wa kuwajibika, kuimarisha nidhamu ya utumishi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya umma, "alisema Jaji Mwangesi.


Alisema viongozi wenye maadili wanapotenda kwa haki, uwazi na uadilifu wanaongeza utiifu wa sheria na mshikamano na hivyo kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali na taasisi zake 

 

"Maadili ni kinga ya maovu yote na nguzo muhimu ya utawala bora na maendeleo endelevu ya taifa" alisema Kamishna Mwangesi.


Kamishna huyo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma iliyosomwa kwa niaba yake na Kamishna ofisi ya rais tume ya utumishi wa umma Nassor Mnambila, aliwataka viongozi kuwa mabalozi wa maadili kuanzia ngazi ya familia


Mafunzo hayo yanawashirikisha Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri na wakurugenzi wa serikali za mitaa. 


Mshiriki wa mafunzo hayo  Mstahiki Meya wa  Manispaa ya Tabora Gullam Dewji alisema viongozi wenye maadili siku zote wanatoa maamuzi yenye kuzingatia haki.


Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Aidda Haule alisema mafunzo  kwa viongozi hao ni muhimu kwa nia ya kuimarisha Utawala bora.


"Serikali inapoleta miradi ya maendeleo kwa wananchi Halmashauri ndizo zinasimamia utekelezaji wa miradi yote hivyo ni lazima kuwepo na uadilifu katika usimamizi alisema Bi Haule.


Mwisho..

No comments: