![]() |
| Katibu wa Siasa,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Pwani David Mramba |
Na Julieth Mkireri.MAIPAC KIBAHA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimesema kinatambua mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo ya Mkoa ikiwa ni pamoja naona fedha za miradi ya maendeleo ambazo zimekuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi.
Katibu wa Siasa,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Pwani David Mramba, amesema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake mkutano uliofanyika Aprili 02/2026.
Amesema mchango huo imesababisha chama hicho kusimama hadharani na kumpongeza Rais Samia kwa namna ambavyo ameung'arisha mkoa huo.
Mramba, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 Mkoa wa Pwani ulitengewa kiasi cha Sh.bilioni 473 fedha ambazo zilitumika kuleta maendeleo ndani ya Mkoa wa Pwani.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali kupitia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeongeza fedha za maendeleo na kupanga kutumia kiasi cha Sh.bilioni 497.1.
Kadhalika Mramba amesema sekta ya maji ilikuwa na changamoto ya kukatika katika kwa maji kulikosababishwa na ubadilishaji wa pamu jambo ambalo kwasasa limetatuliwa .
Ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kujenga miradi ya kuwezesha vijiji vinapata maji safi na salama huku wanawake wakipunguziwa adha ya kubeba maji kwenye ndoo umbali mrefu.
Kuhusu elimu Mramba amesema kuwa Serikali imetoa fedha ambazo zimetumika kujenga madarasa mapya yaliyokamilika,maabara zimejengwa sambamba na vyoo vya Shule kuboreshwa na kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira mazuri zaidi kuliko zamani.
Mramba ameongeza kuwa katika sekta ya afya huduma zimeimarika kwa Zahanati na vituo vya afya kujengwa huku huduma za mama na mtoto zikiimarika na kufanya wananchi kupata huduma karibu na makazi yao.
Tulizo Anton mkazi wa Muheza kata ya Mailimoja ameomba Serikali kusaidia katika eneo la maji kwa sekta inayohusika kuimarisha miundombinu itakayowakwamua kutoka kwenye adha ya kukatika maji kwa muda mrefu.
Naye Amina Mohamed amesema Serikali inatakiwa kuongeza fedha katika sekta ya miundombinu ya barabara ili kuboresha barabara za kwenye mitaa na zile za mchepuko kupunguza foleni katika barabara kuu ya Chalinze Morogoro.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment