DC MWENDA ATOA WITO KWA WALIMU KUTILIA MKAZO MALEZI YA WANAFUNZI. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 30 April 2026

DC MWENDA ATOA WITO KWA WALIMU KUTILIA MKAZO MALEZI YA WANAFUNZI.

MKUU wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, akimkabidhi mmoja wa walimu waliofanya vizuri mtihani ya kitaifa 2025


NA: SEIF TAKAZA, IRAMBA


maipacarusha20@gmail.com


MKUU wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, ametoa wito kwa walimu kuzingatia malezi ya wanafunzi sambamba na utoaji wa elimu darasani.




Mwenda ametoa wito huo katika hafla ya utoaji motisha kwa walimu waliofanya vizuri kitaaluma kwenye mitihani ya kidato cha pili, nne na sita kwa Wilaya ya Iramba iliyofanyika katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, ambapo alibainisha kuwa walimu wana nafasi kubwa katika kujenga jamii iliyo bora.




“Mafanikio ya mwanafunzi hayapimwi kwa ufaulu wa kitaaluma pekee, bali pia kwa mwenendo na tabia njema ya mwanafunzi huyo” alisisitiza Mwenda




Sambamba na hayo, Mwenyekiti wa Huduma za Jamii na Diwani wa Kata ya Tulya, Wilfred Kizanga, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, amesema Wilaya imeweka mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu ili kuongeza ufaulu.




Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora, amewapongeza walimu waliofanya vizuri, akifafanua kuwa zawadi walizopewa si malipo bali ni ishara ya kuthamini jitihada zao katika kuwapatia wanafunzi elimu.




Naye Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Iramba, Mwalimu Diana Sonno, akiwasilisha taarifa ya ufaulu wa mwaka 2025, amesema ufaulu wa kidato cha nne umeongezeka kwa asilimia 0.7, huku kidato cha sita ukiongezeka hadi asilimia 100.




Jumla ya walimu 48 wa masomo mbalimbali wametunukiwa zawadi baada ya kuwa na wanafunzi wengi waliopata daraja A, B na C katika mitihani ya taifa ya kidato cha pili, nne na sita kwa mwaka 2025. Aidha, shule 9 zimepatiwa tuzo maalum kwa kutokuwa na daraja sifuri (0) katika matokeo ya kidato cha nne mwaka huo.

MWISHO

No comments: