Diwani Longido Akamatwa na Mirungi, DCEA Yakamata Zaidi ya Kilo 1,983.31 mwezi Machi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 14 April 2026

Diwani Longido Akamatwa na Mirungi, DCEA Yakamata Zaidi ya Kilo 1,983.31 mwezi Machi


Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo


Na Mwandishi Wetu, maipac


maipacarusha20@gmail.com



Diwani wa Kata ya Kimokouwa wilayani Longido mkoani Arusha, Solomon Koholo (38), amekamatwa akidaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa kilogramu 106.25.  Tukio hilo pia lilimhusisha mtuhumiwa mwenzake Lekaneti Kukuu (38).


" Dawa hizi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish yenye namba ya usajili T 889 DPG, mbali na tukio hili, katika mkoa huo kilogramu 138.42 za mirungi zilikamatwa katika matukio mengine"Kamishna Lyimo



Akitoa taarifa hapo jana, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, alisema katika mwezi Machi 2026 mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.



Alisema sambamba na ukamataji huo, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, huku watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo. Aidha, magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa.


Kwa mujibu wa Kamishna Lyimo, uchambuzi wa takwimu umebaini ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo.


Alieleza kuwa hali hiyo imetokana na mkakati wa mamlaka kujikita katika operesheni za dawa za kulevya za mashambani baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.


Akielezea matukio mbalimbali, alisema jijini Dar es Salaam katika eneo la Tegeta Kibo, kilogramu 101.2 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa katika basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lenye namba ya usajili T 181 EMJ, lililokuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania. Dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC).


Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva Ramadhan Mohamed (52), Salma Sanga (26) kondakta, pamoja na Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39).



Mkoani Pwani, kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam.


Mkoani Mwanza, kilogramu 52 za mirungi zilikamatwa katika kizuizi cha barabarani cha Magu pamoja na Bandari ya Mwanza South, zikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso lenye namba ya usajili T 296 APA, zikiwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba. Dereva wa gari hilo, Hassan Hassan (37), alikamatwa.


Aidha, wilayani Misungwi mkoani humo, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa zikiwahusisha Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55). Dawa hizo zilibainika ndani ya nyumba na katika vyombo vya usafiri ambavyo ni gari aina ya Toyota Crown lenye namba ya usajili T 742 EGL, Toyota Wish yenye namba ya usajili T 854 DXB pamoja na bajaji yenye namba za usajili MC 261 EZV.


Mkoani Tanga, kilogramu 32.95 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya mfuko kwa kuchanganywa na maembe. Katika tukio hilo, Seif Omar (38), maarufu kwa jina la Haniwao, alikamatwa. Katika operesheni nyingine mkoani humo, jumla ya kilogramu 164.01 za mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti.


Kadhalika, mkoani Kilimanjaro katika maeneo ya Himo na Same, kilogramu 68.3 za mirungi zilikamatwa zikiwahusisha watuhumiwa Amin Mazua (58) maarufu kwa jina la Mbaruku na Wilbard Mchau (50).

Sambamba na udhibiti wa mirungi, aina nyingine za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini. Jijini Dar es Salaam, katika hosteli ya wanafunzi iliyopo mtaa wa Nzasa, Kijitonyama, zilikamatwa paketi 141 za bangi aina ya skanka, ambapo mtuhumiwa Semvua Sangi (31) alikamatwa.


Aidha, mkoani Songwe katika eneo la Tunduma, kilogramu 8.2 za bangi aina ya skanka zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa na mtuhumiwa Lwitiko Kapambila (39) kuelekea Mbeya mjini.


Katika operesheni nyingine zilizofanyika nchini jumla ya kilogramu 707.995 za bangi zilikamatwa.


Kamishna Lyimo alisema katika kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu na kuzuia uchepushwaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya, mamlaka ilifanya ukaguzi katika kampuni zinazojihusisha na kemikali bashirifu, maduka ya dawa, kampuni za usafirishaji vifurushi na bandari kavu.


Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo



Kupitia ukaguzi huo, jumla ya kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu zilikamatwa kutokana na kukiuka taratibu za kisheria, zikiwemo Potassium permanganate, Hydrochloric acid, Acetone, Sulphuric acid na Acetic acid glacial.


Aidha, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa, zikiwemo alprazolam, midazolam, clonazepam, fentanyl, zolpidem, tramadol, codeine na dihydrocodeine.

Alibainisha kuwa kitaalam dawa hizo hujumuisha makundi ya Benzodiazepini, dawa za kutuliza na kusababisha usingizi pamoja na dawa zenye asili ya afyuni zinazotumika kutibu maumivu, na zisipotumika ipasavyo zinaweza kusababisha uraibu.

Kwa ujumla, alisema operesheni za mwezi Machi 2026 zimeakisi dhamira thabiti ya Serikali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya nchini, huku akibainisha uwepo wa mitandao mipya ya usafirishaji wa dawa hizo hususan mirungi pamoja na mabadiliko ya mbinu za usafirishaji ili kukwepa kubainika.

Alisisitiza kuwa DCEA itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi nyingine za udhibiti pamoja na wananchi ili kudhibiti mianya yote inayoweza kutumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahusika.


Mwisho.

No comments: