KAMUGISHA ATOA WITO KWA WAENDESHAJI USAILI KUZINGATIA UADILIFU ‎ - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 14 April 2026

KAMUGISHA ATOA WITO KWA WAENDESHAJI USAILI KUZINGATIA UADILIFU ‎

 





Na mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com 


‎Makamu Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Uhamiaji, Said Abeid Kamugisha, amewataka waendeshaji wa mchakato wa usaili wa Ajira serikalini kutanguliza maslahi ya Taifa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu katika zoezi la kuwachuja waombaji kazi.

‎Wito huo umetolewa Aprili 13, 2026, jijini Arusha wakati wa kikao kazi kilicholenga kutoa mwongozo wa uendeshaji wa usaili kwa Vijana walioitwa kwenye usaili  kinachofanyika katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

‎Kamugisha amesisitiza kuwa wataalamu kutoka kada mbalimbali wanapaswa kufanya maamuzi sahihi bila upendeleo wowote, ili kupata watumishi wenye sifa stahiki watakaosaidia kulijenga Taifa.

‎Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya Ajira, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali katika mchakato wa Usaili. Amesema hatua hiyo imepunguza urasimu, kuondoa mianya ya upendeleo, pamoja na kupunguza usumbufu kwa waombaji kazi.

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Beni Kalage, amesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa nyaraka muhimu, ikiwemo vyeti vya taaluma na uthibitishaji wa majina ya waombaji, ili kuzuia udanganyifu.

‎Kalage pia amebainisha kuwa makundi yenye mahitaji maalum yatapewa kipaumbele, wakiwemo watu wenye ulemavu, wagonjwa pamoja na wanawake wajawazito, huku akisisitiza kuwa zoezi la Usaili hufanyika kwa kuzingatia Sheria,Kanuni, taratibu  na Miongozo ya Utumishi wa Umma.

‎Naye Afisa Utumishi wa Mkoa wa Arusha, Catherine Thomas, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Toba Nguvila, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya usahili na Ajira. ambapo Amesema uwepo wa vituo vya usajili katika kila Mkoa umepunguza gharama za usafiri kwa vijana na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa njia ya kidijitali.

‎Mwisho.

No comments: