JOWUTA yashiriki kikao Meimosi ,yataka ushirikishwaji zaidi wanahabari - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 15 April 2026

JOWUTA yashiriki kikao Meimosi ,yataka ushirikishwaji zaidi wanahabari

Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma








Mwandishi wetu,Njombe.


maipacarusha20@gmail.com 


Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA), kimetaka ushirikishwaji zaidi wa vyombo vya habari katika maadhimisho ya kitaifa ya Mei Mosi mkoani Njombe.


JOWUTA inashiriki Mei Mosi yake ya kwanza mwaka huu kama mwanachama wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA) na inatarajia kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora katika vyombo vya habari.


Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma licha ya kupongeza Kamati ya Habari na Matangazo ya Mei Mosi kitaifa, alisema bado ushiriki wa vyombo vya habari sio mkubwa.


Juma alisema, Kamati hiyo inapaswa kuvishirikisha zaidi vyombo vingi vya habari ikiwepo mitandao ya kijamii, Magazeti, Luninga na Radio kuwapa habari na matangazo.


"Lakini pia ni muhimu maudhui ya matangazo yalenge kuonesha vitu vya kipekee vilivyopo mkoa wa Njombe" alisema

Juma aliahidi JOWUTA yenye wanachama wanahabari zaidi ya 400 nchi nzima ipo tayari kushirikiana na kamati za Mei mosi kuongeza kazi za utangazaji na kuelezea umuhimu wa watanzania kushiriki maadhimisho hayo.


Naye Mwenyekiti wa Taifa wa RAAWU, Jane Mihanji alikumbusha kamati  hiyo kukumbuka umuhimu wa kugharamia magazeti ambayo yamekuwa yakitoa matoleo maalum ya Mei mosi kwa wakati.


"Matoleo haya ikiwepo jarida Uhuru wa kijani yamekuwa yakitoa makala maalum za utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya serikali na sekta binafsi na kugawanywa bure wa maelfu ya watu siku ya Mei Mosi "alisema


Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya alisema ,Njombe ina vitu vingi vya kuvitangaza kupitia maadhimisho ya Mei Mosi


"Mei mosi ni fursa kwa wakazi mkoa Njombe kuna mengi ya kutangaza mkoa huu ikiwepo kilimo kikubwa cha maparachichi, viazi mbatata, mbao na maporomoko ya maji na Utalii"alisema.


Wakati huo huo, Kamati ya maandalizi ya Mei mosi kitaifa imetembelea maandalizi ya ujenzi wa uwanja Mei Mosi na kutaka kasi zaidi iongezwe ili ukamilike ifikapo Aprili 25 mwaka huu.


Mwisho.




 



No comments: